1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON:Bodi kuamua hatma ya Paul Wolfowitz

15 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC1w

Bodi kuu ya Benki ya Dunia inaamua hii leo iwapo kiongozi wa benki hiyo Paul Wolfowitz anaendelea kushikilia wadhifa wake.Taarifa iliyotolewa na Kamati maalum ya benki hiyo inapendekeza kuwa wakurugenzi kuzingatia uwezo wa Bwana Wolfowitz ili kutimiza malengo ya Benki ya Dunia.

Bodi hiyo iliyo na wanachama 24 inakutana hii leo huku Bwana Wolfowitz akishutumiwa kwa kumwongeza mshahara mpenzi wake kinyume na sheria Bi Shaha Riza ambaye pia ni mfanyikazi wa benki hiyo.

Paul Wolfowitz aliye na umri wa miaka 63 alikuwa afisa wa ngazi za juu katika Idara ya Ulinzi vilevile mshirika mkuu katika mpango wa Marekani kuvamia Iraq anatarajiwa kujitetea mbele ya bodi hiyo.Kamati maalum inayofanya uchunguzi wa kashfa hiyo imeshaamua kuwa Bwana Wolfowitz alikiuka maadili ya shirika hilo alipomwongeza mshahara Bi Shaha Riza mwaka 2005 alipojiunga na Benki hiyo.

Kashfa hiyo imesababisha mgawanyiko mkubwa katika mataifa wanachama wa Benki ya Dunia huku Marekani ikimuunga mkono Bwana Wolfowitz kwa upande mmoja na Mataifa ya Ulaya kushikilia kuondolewa kwake.Kiongozi wa Benki hiyo huteuliwa kwa kawaida na Marekani.