1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON.Bush akabiliwa na miito ya kumtaka afikirie upya kuhusu Irak

23 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD03

Rais George Bush wa Marekani anakabiliwa na miito ndani ya nchi yake inayomtaka kufikiria upya sera za serikali yake kuhusu Irak baada ya rais huyo kusema kuwa anazingatia kubadili mkakati wa kijeshi nchini humo.

Idadi ya watu wanouwawa nchini Irak imeongezeka huku uchaguzi wa baraza la congress ukikaribia kufanyika.

Bwana John Warner wa chama cha Republican cha rais Bush anaeongoza idara ya ulinzi katika baraza la Senate amekiri kupitia televisheni ya Fox kwamba hali nchini Irak ni tete na inazidi kuwa mbaya.

Wakati huo huo Afisa wa cheo cha juu katika jeshi la Marekani Alberto Fernandez akizungumza na kituo cha televisheni cha Al Jazeera amekiri kuwa nchi yake haikufikiria vyema kabla ya kuivamia Irak.

Ikulu ya White House hata hivyo imekanusha kauli ya hiyo na kusema kuwa imetangazwa kinyume na afisa Fernandez alivyosema.

Katika mashambulio mapya ya mabomu mjini Baghdad watu watano wameuwawa katika eneo la maduka.

Ripoti ya makamanda wa jeshi la Marekani imesema kuwa katika mwezi huu wa oktoba pekee jeshi hilo limewapoteza wanajeshi wake 79.