1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON:Rais Bush atangaza kupeleka askari zaidi Iraq,akubali lawama pale yalipotokea makosa

11 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCbs

Rais George Bush wa Marekani ametangaza kuongeza zaidi ya askari elfu 20 nchi ni Iraq, na pia amekubali kubeba lawama pale makosa yalipotokea katika siasa zake nchini humo.

Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni dakika chache zilizopita Rais Bush pia ameitaka serikali ya Iraq kutimiza ahadi yake ya kupambana na ghasia za wapiganaji wa kisunni, vinginevyo itanyimwa msaada na Marekani.

Amesema kuwa idadi kubwa kati ya hao watakaopelekwa nchini Iraq watakuwa jijini Baghdad, kusaidia urejeshwaji wa usalama na wengine katika jimbo la Anbar.

Rais Bush pia amezilaumu Iran na Syria kwa kuwasaidia wapiganaji wa kisunni na kwamba Marekani itazuia misaada yoyote kutoka nchi hizo kwenda Iraq.

Akizungumza kutoka katika maktaba yake ya Ikulu ya Marekani, Rais Bush ameonya ,kuwa kushindwa kwa Marekani nchini Iraq itakuwa adhaa kubwa na kutatoa mwanya kwa makundi ya kigaidi kuhatarisha eneo lote la mashariki ya kati.

Rais Bush pia amesema kuwa serikali yake itashirikiana na serikali ya Uturuki katika kuimarisha usalama kwenye mpaka wa nchi hiyo na Iraq.

Mapema ilidokezwa kuwa Rais Bush ataomba aidhinishwe kiasi cha dola billioni 6.8 za ziada kugharimia kikosi hicho pamoja na kusaidia uchumi wa Iraq.

Lakini Chama Democrat ambacho kwa sasa kina idadi kubwa katika bunge la Congress kimesema kuwa hakitaunga mkono uidhinishwaji wa kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya askari wa ziada.

Mara baada ya hotuba hiyo Seneta Barack Obama mtu anayetegemewa kuwa mgombea urais katika uchaguzi ujayo alisema kuwa Rais Bush alitakiwa kutangaza mikakati ya kisiasa zaidi kuliko ya kijeshi.

Seneta mkongwe wa Democrat Edward hapo juzi alisema kuwa kutuma askari wa ziada nchini Iraq ni kosa jipya ambalo ni kubwa.Marekani kwa sasa ina kiasi cha askari laki moja na elfu 32.

Mjini Seol Rais Roh Moo-hyun wa Korea Kusini amesema kuwa ana muunga mkono Rais Bush katika mikakati yake hiyo ya kuongeza askari zaidi nchini Iraq.

Rais huyo wa Korea Kusini alisema hayo wakati wa mazungumzo yake kwa njia ya simu na Rais Bush muda mfupi kabla Rais Bush hajatoa hotuba yake.Korea Kusini ina askari 2,300 kaskazini mwa Iraq katika mji wa Irbil

Mjini London Waziri Mkuu wa Uingereza Tonny Blair ambaye ni mfuasi mkubwa wa Rais Bush alikataa kuelezea iwapo atafuata nyayo za Rais Bush katika kuongeza idadi ya askari wake nchini Iraq.Uingereza ina askari 7500 huko kusini mwa Iraq.

Wakati huo huo nchini Iraq watu wenye silaha wameushambulia msafara wa mahujaji wa kishia na kuwaua 11 huku wengine 14 wakijeruhiwa.

Wizara ya mambo ya ndani ya Iraq imesema kuwa mahujaji hao walikuwa wakirudi kutoka katika hijaa nchini Saudi Arabia.