1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha CSU chapata pigo uchaguzi wa jimbo la Bavaria

Josephat Charo
14 Oktoba 2018

Chama cha kihafidhina cha Christian Social Union, CSU, ambacho kilikuwa kikilitawala jimbo la Bavaria kusini mwa Ujerumani kimepata pigo la kihistoria kwa matokeo ya kufedhehesha katika uchaguzi wa Jumapili (14.10.2018)

https://p.dw.com/p/36Wy2
Bayern Landtagswahl  Söder und Seehofer
Horst Seehofer, mwenyekiti wa cha chama cha CSU, kushoto, na Markus Södner, waziri mkuu wa jimbo la BavariaPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Chama cha Christian Social Union, CSU, ambacho ni chama mshirika wa chama cha kansela wa Ujerumani Angel Merkel cha Christian Democratic Union, CDU, kimepata matokeo mabaya kabisa katika historia ya uchaguzi tangu mwaka 1950 katika uchaguzi uliofanya Jumapili (14.10.2018) katika jimbo la kusini mwa Ujerumani la Bavaria. Chama hicho kimepoteza kura kwa chama cha mrengo wa kulia katika pigo ambalo linatishia kuongeza mipasuko katika serikali kuu ya mseto ya Ujerumani inayozongwa na mzozo.

Huku kura zote zikiwa zimeshahesabiwa, chama hicho cha kihafadhina jimboni Bavaria pamoja na mshirika wake chama cha Social Democratic ndivyo vilivyopata fedheha kubwa katika uchaguzi wa bunge la jimbo la Bavaria mjini Munich.

Kwa mujibu wa maokeo rasmi ya awali chama cha CSU kimepoteza asilimia kumi ya uungwaji mkono huku asilimia 37.2 tu ya wapiga kura wakikichagua chama hicho. Chama cha Social Democratic, SPD, chama cha tatu mshirika katika serikali ya mseto katika ngazi ya shirikisho pamoja na chama cha kansela Merkel cha Christian Democratic Union, CDU, kimepata asilimia 9.7 ya kura, ikiwa ni takriban nusu ya kura walizopata katika uchaguzi wa 2013.

Chama cha Kijani chajiimarisha Bavaria

Chama cha Kijani kimeshika nafasi ya pili katika uchaguzi wa Bavaria kwa kujikingia asilimia 17.5 ya kura, matokeo yanayodhihirisha chama hicho kimejiimarisha kwa takriban pointi nane. Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, Chama Mbadala kwa Ujerumani, AfD, kimepata asilimia 10.2 ya kura na hivyo kitawakilishwa katika bunge la Bavaria kwa mara ya kwanza.

Landtagswahl in Bayern Die Grünen
Robert Habeck wa chama cha Kijani akisalimiana na wenzake kabla matokeo ya awali kutangazwa katika kituo cha televisheni cha umma nje ya jengo la bunge mjini Munich 14.10.2018Picha: Getty Images/AFP/O. Andersen

Chama cha wapiga kura huru, Freie Waehler, kimeshinda asilimia 11.6 ya kura huku chama cha kiliberali kinachowapendelea wafanyabiashara Free Democratic, kikiwa kimepata asilimia asilimia 5.1 kuweza kuwakilishwa tena katika bunge hilo. 

Matokoe ya utafiti wa maoni uliofanywa na kituo cha utangazaji cha Ujerumani, ARD, muda mfupi baada ya upigaji kura kukamilika chama cha CSU kilikuwa kimeshinda asilimia 35.5 ya kura. Chama hicho kimepoteza wingi wake wa wajumbe bungeni kwa mara ya pili tangu mwaka 1962, matokeo ambayo kwa hakika yatachochea mivutano ndani ya chama, ambacho tayari kimegeuka kuwa mshirika mbaya na mgumu wa kansela Merkel katika serikali kuu ya shirikisho mjini Berlin.

Matokeo hayo, ambayo yameshuhudia chama cha walinda mazingira Die Grüne kikishika nafasi ya pili na chama cha mrengo wa kulia, chama Mbadala kwa Ujerumani, AfD, kikiingia katika bunge la jimbo la Bavaria kwa mara ya kwanza, yana maana chama cha CSU kitahitajika kuunda serikali ya mseto - hatua ambayo ni fedheha kwa chama kilichozowea kutawala peke yake jimboni Bavaria.

Mwandishi: Josephat Charo/rtre/afpe/dpae