1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasifu wa Simba Makoni

28 Machi 2008

Simba Makoni mgombea wa urais nchini Zimbabwe atowa changamoto ya kijasiri kwa Rais Robert Mugabe anayetetea wadhifa wake.

https://p.dw.com/p/DWTV
Kutokana na hali mbaya ya uchumi mamia ya watu hufurika madukani mjini Harare kugombania bidhaa.Picha: AP

Kutimuliwa kwa Simba Makoni katika chama tawala cha Robert Mugabe kunaashiria changamoto kubwa kabisa ya ndani ya chama inayomkabili rais huyo wa Zimbabwe tokea aingie madarakani na inaonyesha kuwepo kwa mgawanyiko kwenye kambi ya kiongozi huyo mkongwe.

Makoni amejitokeza kwa ujasiri kumpinga Mugabe katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo hapo kesho. Lakini Makoni ambaye Mugabe amemshutumu kuwa kahaba wa kisiasa yumkini kijasho kikubwa kikamtoka katika uchaguzi huo wa rais baada ya kampeni za wiki chache na kwa kuzingatia ukweli kwamba vigogo wa chama tawala cha ZANU-PF ambao ilivuma kwamba wanamuunga mkono wameshindwa kujitokeza hadharani.

Akionekana kuwa ni mwanamageuzi ambaye hakuguswa na kashfa za rushwa waziri huyo wa fedha wa zamani amejitetea kutokana na shutuma kwamba anastahiki kulaumiwa kwa maafa ya kiuchumi yalioikumba nchi hiyo wakati akiwa mshirika wa Mugabe.

Kama vile wagombea wengine amefanya suala la kufufuwa uchumi kuwa kitovu cha kampeni yake.

Lakini tafauti na mikutano mikubwa ya hadhara ya Mugabe na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai Makoni ameweza kuvutia umma mdogo tu licha ya kwamba umma huo ulikuwa umejawa hamasa.

Pia ana kasoro za sifa za upinzani za Tsvangirai ambaye akiwa kiongozi wa kundi kuu la chama cha MDC ameweza kuhimili mapigo ya ukandamizaji ya Mugabe moja baada ya jengine.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mpinzani wa Mugabe John Makumbe akizungumzia juu ya nafasi za Makoni kushinda uchaguzi huo amesema yumkini kabisa akazigawa kura za ZANU-PF na kusababisha chama cha MDC kiibuke mshindi juu ya kwamba wachambuzi wengine wanaamini kwamba anaweza kuvutia umma katika nchi hiyo iliogawika kisiasa.

Makoni mara ya kwanza alikorofishana na Mugabe hapo mwaka 2002 wakati alipojiuzulu waziri wa fedha katika mzozo juu ya namna ya kukabiliana na matatizo ya kiuchumi yaliokuwa yakizidi kuongezeka kila uchao.

Makoni alikuwa akishinikiza kushushwa thamani kwa sarafu ya Zimbabwe jambo ambalo limemfanya ashutumiwe na Mugabe kwa kutaka kuhujumu uchumi.

Licha ya kutohusishwa na rushwa ambako kumewagusa karibu washirka wote wa karibu wa Mugabe jambo hilo halikuweza kumhifadhi dhidi ya mdomo wa kifedhuli wa Mugabe ambaye amemwita kahaba wa kisiasa na chura aliefura.

Hata hivyo Makoni ambaye alikuwa waziri kijana kabisa katika serikali ya kwanza ya Mugabe mara baada ya kupata uhuru amekataa kujihusisha na kampeni za kutukanana.

Badala yake amemuelezea Mugabe Mugabe kuwa ni mtu mwenye nafasi maalum katika historia yao.

Makoni ambaye hapo tarehe 26 mwezi huu wa Machi ametimiza miaka 58 alijifunza kemia nchini Uingereza.

Wakati wa uhuru wa nchi hiyo hapo mwaka 1980 alichaguliwa kuwa waziri kilimo na pia amewahi kushika nyadhifa mbali mbali kabla ya kuwa katibu mkuu mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi ya nchi za kusini mwa Afrika SADC wadhifa alioushikilia kwa miaka tisa.