1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi wa kufanyika mkutano wa Korea mbili

Admin.WagnerD23 Mei 2018

Waandishi habari wa kimataifa walioalikwa na  Korea kaskazini, wamekusanyika hii leo  kushuhudia kuharibiwa kwa eneo la majaribio ya Nyuklia  la taifa hilo.

https://p.dw.com/p/2yBEN
Nordkorea - Ausländische Reporter zur Atomtestgelände-Sprengung in Nordkorea angekommen
Waandishi wa habari waliokusanyika kushuhudia kuteketezwa silaha za nyukliaPicha: picture-alliance/AP/kyodo News

Tukio hilo  linaangaliwa  kuwa ni hatua  njema kuelekea mkutano wa kilele unaotarajiwa kufanyika  mwezi ujao, kati ya rais Donal Trump wa Marekani na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, licha ya shaka shaka ziliopo. Kuharibiwa kwa eneo hilo la majaribio ya nyuklia kunatarajiwa kufanyika  kati ya leo Jumatano na Ijumaa, ikitegemea hali ya hewa. Korea Kaskazini inaichukulia hatua yake hiyo  kuwa ni ya moyo mwema, kabla ya mkutano huo wa kilele uliopangwa kufanyika Juni 12 nchini Singapore.

Mashaka ya kufanyika mkutano wa kilele wa Korea Kaskazini na Kusini

Lakini  pande zote mbili zimeelezea shaka shaka  iwapo kweli mkutano huo wa kihistoria utafanyika. Korea Kaskazini ilitishia kujiondoa ikiwa Marekani itaishinikiza iachane na shughuli zake za kinyklia. Pia Trump alisema baada ya kukutana na  Rais wa Korea Kusini Moon Jae-In jana Jumanne mjini washington, kwamba mkutano wake na Kiongozi wa Korea Kaskazini unaweza ukacheleweshwa. Baadaye aliwaambia waandishi habari kwamba  Kuna masharti fulani ambayo Marekani inataka yatimizwe. Alisema anafikiri masharti hayo yatatekelezwa  la sivyo hapatokuweko na mkutano unaotarajiwa. Trump hakufafanua juu ya masharti hayo.

USA Präsident Donald Trump & Moon Jae-in, Präsident Südkorea
Marais Donald Trump na Moon Jae-in mjini WashingtonPicha: Getty Images/W. McNamee

Jitihada za Trump za kukutana na Kim Jong Un

Kisiasa  Trump amefanya juhudi kubwa ili mkutano wake wa kilele na Kim ufanikiwe, na faraghani maafisa wa marekani na pia  waangalizi wa kigeni wanaamini utafanyika kama ulivyopangwa. Lakini wakati siku zikizidi kusogea kuelekea Juni 12, kuna hali ya wasiwasi na tafauti zilizopo kati ya  pande hizo mbili zinazidi kujitokeza. marekani imeeleza wazi inataka Korea Kaskazini iachane na  shughuli zake za kinyklia, na Korea kaskazini imekula kiapo kwamba  haitofanya hivyo hadi ina uhakika  iko salama kutokana na kile inachokiona kuwa ni uchokozi wa Marekani. Awali waandishi habari kutoka Korea Kusini waliachwa nyuma kwa kuwa hawakupata kibali kutoka PyongYang. Hata hivyo Wizara ya Korea Kusini inayohusika na suala la muungano wa korea mbili, ilisema waandishi  hao  sasa wameruhusiwa, kushiriki katika dakika ya mwisho.

Waangalizi watashuhudia kuharibiwa kwa eneo la majaribio ya Kinyuklia. Wakosoaji wanasema  eneo hilo tayari halina  maana baada ya kutumiwa kwa majaribio 6 hapo kabla , hata hivyo ikihitajika linaweza kuandaliwa kwa majaribio mengine. Waandishi habari kutoka China, marekani na Urusi walisafiri kwa ndege ya kukodi jana kutoka Beijing hadi mji wa  Korea kaskazini wa Wonson. Kutoka huko wanatarajiwa kusafiri kwa muda wa masaa 20 kwa treni na basi  hadi mwambao wa mashariki.

Wakati hayo yakijiri , Wizara ya mambo ya nchi za nje ya China , imesema leo kwamba nchi hiyo imetoa mchango mkubwa katika rasi ya Korea na inamatumaini mkutano wa kilele kati ya Marekani na Korea Kaskazini unaweza kufanyika. taarifa ya Wizara hiyo ilitolewa katika kikao cha kawaida na waandishi habari. Jana Rais Trump wa Marekani alirejea  tena matamshi yake kwamba  anafikiri mkutano wa karibu kati ya Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na rais Xi Jinping wa China ulimshawishi Kim kuwa na msimamo mkali kabla ya mkutano wake na Trump.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp rtr
Mhariri: Iddi Ssessanga