1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi wa vikwazo zaidi dhidi ya Guinea.

Halima Nyanza21 Oktoba 2009

Mzozo wa kisiasa nchini Guinea umezidi kuchukua sura mpya kimataifa, baada ya Marekani kuunga mkono hatua ya Jumuia ya ECOWAS, kuiwekea vikwazo nchi hiyo, huku Umoja wa Ulaya ukiahirisha makubaliano ya maelfu ya yuro.

https://p.dw.com/p/KBl4
Kapteni Moussa Camara, utawala wake wa Kijeshi nchini Guinea, hatarini kukumbwa na vikwazo zaid.Picha: AP

Wakati wasiwasi wa nchi hiyo kukumbwa na vikwazo zaidi ukiongezeka, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Alexandre Cece Loua amefanya ziara katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita, mjini The Hague, Uholanzi, na kuzunguzia mauaji ya watu wengi waliokuwa wakishiriki katika mkutano wa upinzani nchini humo mwezi uliopita.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mwendesha mashtaka imesema Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Guinea amekutana na msaidizi wa Mwendesha mashtaka Fatou Bensouda kuzungumzia suala hilo pamoja na hatua zinazochukuliwa na Guinea kwaadhibu wale wote waliohusika na uhalifu huo.

Mapema mwezi huu Ofisi ya Mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa Kivita ya The Hague ilianza kufanya uchunguzi wa awali kuhusiana na machafuko hayo yaliyotokea Septemba 28 ili kuamua kama madai hayo ya uhalifu, yanaendana na sheria za mahakama hiyo.

Kwa upande wake, kiongozi wa utawala wa kijeshi wa Guinea Moussa Dadis Camara ameunda pia tume hutu kuchunguza mauaji hayo ambayo itafanya kazi sambamba na Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa.

Kufuatia tukio hilo la mauaji ya Septemba 28, yaliyotokea baada ya wanajeshi wa Guinea kuufyatulia risasi umati wa watu waliokuwa wakihudhuria mkutano wa upinzani kuupinga utawala wa kijeshi wa nchi hiyo, ambapo Umoja wa Mataigfa unakadiria kuwa watu wapatao 150 waliua na uamuzi wa Jumuia ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi -ECOWAS-, ambayo tayari imeisimamisha Guinea uanachama, kuiwekea vikwanzo vya silaha nchi hiyo baada ya utawala huo wa kijeshi kujaribu kununua silaha zaidi, Marekani nayo imesema inaunga mkono vikwazo vya silaha ilivyowekewa nchi hiyo na jumuia hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani imesema nchi hiyo inaunga mkono kwa nguvu zote Jumuia hiyo ya Ecowas kwa uamuzi wake huo na pia kushirikiana na Umoja wa Afrika kuendeleza utaratibu wa kulenga vikwazo kwa mtu mmoja mmoja.

Kwa upande mwingine Kamishna wa Jumuia ya Uvuvi ya Umoja wa Ulaya Joe Borg amesema ameondoa pendekezo la kuingia ubia na Guinea kwa kusema kuwa litakuwa ni jambo lisilokubalika kisiasa iwapo wataendelea na mpango huo.

Pendekezo hilo ni la makubaliano yaliyofikiwa kwa mara ya kwanza Desemba mwaka jana ya ushirikiano kuhusiana na kuvua samaki aina ya Jodari pekee.

Makubaliano ambayo yangeruhusu Guinea kupatiwa msaada wa takriban Yuro elfu 450 kwa mwaka kusaidia sekta ya uvuvi ya nchi hiyo na yuro nyingine milioni 1.6 katika kipindi cha miaka minne kuendeleza mfumo katika kudhibiti zaidi vitendo vya uvuvi.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri:Mtullya Abdu