1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi watanda Kinshasa

21 Januari 2015

Milio ya risasi imesikika leo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ambako wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kinshasa, wanaandamana kupinga pendekezo la marekebisho ya sheria inayoweza kuchelewesha uchaguzi wa rais mwakani.

https://p.dw.com/p/1ENf4
Moja ya eneo la Kinshasa lililo na kizuizi
Moja ya eneo la Kinshasa lililozingirwa na kizuiziPicha: Reuters/J. R. N'Kengo

Maandamano hayo ya umma yaliyoitishwa na vyama vya upinzani kwa lengo la kupinga hatua ya bunge kupitisha kipengele cha katiba kitakachorefusha uchaguzi wa rais wa mwaka ujao wa 2016, ambacho kinajadiliwa katika vikao vya Baraza la Seneti. Upinzani unamtaka Rais Joseph Kabila, ambaye amekuwepo madarakani kwa miaka 14 sasa, kuachia nafasi hiyo pindi kipindi chake kitakapomalizika mwaka ujao wa 2016.

Milio hiyo ya risasi ilisikika wakati ambapo mamia ya wanafunzi waliokuwa wakiandamana leo huku wakipiga kelele wakisema ''Kabila ondoka madarakani!'', walipokutana na kundi dogo la askari polisi. Katika eneo la Ndjili, vijana waliliharibu gari moja la polisi.

Kiongozi wa upinzani, Etienne Tshisekedi
Kiongozi wa upinzani, Etienne TshisekediPicha: AP

Mjini Brussels, Ubelgiji, kiongozi wa upinzani, Etienne Tshisekedi, amewasihi watu wa Kongo kufanya kila jitihada kuundoa madarakani ''utawala usio na manufaa.'' Tshisekedi ambaye anatibiwa mjini humo, amewataka polisi na wanajeshi kuwalinda raia na kutotekeleza amri wanazopewa, za kuwaua watu wasio na silaha.

Taarifa iliyotolewa na shirika la haki za binaadamu la Kongo, imeeleza kuwa watu 28 wameuawa tangu siku ya Jumatatui katika maandamano hayo ya kuipinga serikali. Hata hivyo, maafisa wa Kongo wanasema kuwa idadi ya watu waliouawa ni watano.

Watu 20 wanashikiliwa na jeshi na polisi

Msemaji wa Serikali ya Kongo, Lambert Mende, amesema askari polisi wawili waliuawa kwa risasi siku ya Jumatatu na wengine wawili waliuawa na waporaji. Polisi na jeshi linawashikilia kiasi watu 20 waliokuwa wanaandamana.

Akizungumzia kuhusu mvutano huu wa pendekezo la mabadiliko ya kifungu cha katiba, yatakayoweza kuuchelewesha uchaguzi wa rais mwaka ujao 2016, kati ya serikali ya Kongo na upinzani, mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Kongo, Fidel Bafilemba, anasema nia ya Rais Kabila ni sawa na kutaka kuizamisha nchi ya Kongo.

Bafilemba ambaye alikuwa akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya DW, amesema, ''Hauwezi kuongoza nchi kwa zaidi ya miaka 14 na ushindwe kujenga jeshi, ushindwe kuendeleza siasa, ushindwe kujenga uchumi, kila kitu Kongo hakiendelei. Na wakati katiba inakwambia wewe una mihula miwili tu na umefika mwisho, sasa Kongo leo inaelekea katika njia mbaya sana, inakuwa kama vile boti inayotaka kuzama.''

Rais Joseph Kabila
Rais Joseph KabilaPicha: Reuters

Hata hivyo, wakosoaji wanasema hatua hiyo ni njama ya Rais Kabila kutaka kuendelea kubakia madarakani. Wanasema serikali inataka kuifanyia marekebisho sheria hiyo ya uchaguzi na kuamuru lifanyike zoezi la kuwahesabu watu nchini humo kabla ya uchaguzi.

Rais Kabila, mwenye umri wa miaka 43, aliingia madarakani Januari mwaka 2001, baada ya baba yake Laurent Kabila kuuawa, na alishinda katika uchaguzi wa mwaka 2006 na 2011. Katiba ya Kongo inamzuia Kabila kugombea katika uchaguzi wa urais kwa muhula wa tatu, hapo mwakani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE,DPAE
Mhariri:Iddi Ssessanga