1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasoshialisti waondolewa patupu Ufaransa

31 Machi 2014

Siku moja tu baada ya wasoshilisti kushindwa vibaya sana katika uchaguzi wa mabaraza ya miji ya Ufaransa,rais Francois Hollande anashinikizwa na kila upande aivunje serikali na abadilishe pia mkondo wa siasa yake.

https://p.dw.com/p/1BYu7
Mji mkuu wa Ufaransa Paris umejipatia meya wa kwanza mwanamke:Anne Hidalgo wa chama cha kisoshialistiPicha: Reuters

"Rais amevuliwa nguo" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la mrengo wa shoto La Liberation linalohisi rais Hollande ambae hapendi kupitisha uamuzi kwa pupa,hawezi tena kukwepa na "anabidi afichue haraka kile anachodhamiria kufanya."

"Zilzala,pigo,adhabu,hatakiwi" ni miongoni mwa vichwa vya maneno katika magazeti ya Ufaransa yanayotoa picha ya janga linalomgubika rais Hollande baada ya uchaguzi huu ambao ni wa kwanza tangu aingie madarakani mwezi Mai mwaka 2012.

Kambi ya wasoshialisti imepokonywa na wahafidhina miji isiyopungua 155 yenye wakaazi zaidi ya 9000-na baadhi ya miji hiyo ilikuwa ikiongozwa na mrengo wa shoto kwa zaidi ya miaka 100.

Sauti zinazidi kupazwa waziri mkuu abadilishwe

Miito kutaka waziri mkuu abadilishwe imezidi kupata nguvu sio tu kutoka kambi ya wahafidhina bali pia mrengo wa shoto. Jean-Marc Ayrault anatwikwa jukumu la kushindwa siasa ya serikali ya Ufaransa tangu takriban miaka miwili iliyopita.Kwa mujibu wa utafiti wa maoni ya wananchi uliosimamiwa na taasisi ya BVA,zaidi ya robo tatu ya wafaransa wasingependelea kumuona Jean Marc Ayrault akiendelea kuongoza serikali.

Hollande, Ayrault und Vallaud-Belkacem
Kutoka kushoto:rais Hollande,waziri mkuu Ayrault na waziri wa masuala ya haki za akinamama ambae pia ni msemaji wa serikali Nadjat Vallaud BelkacemPicha: J.Demarthon/AFP/GettyImages

Wakaribu wa rais Francois Hollande wamesema wazi jana usiku "ujumbe wameupata".Rais Francois Hollande anatazamiwa kulihutubia taifa leo hii."Wapiga kura wameelezea hisia zao...na baadhi ya wakati kwa hasira" amesema hayo waziri wa mambo ya ndani Manuel Valls anaepewa nafasi nzuri ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu mpya.Amekiri matokeo ya uchaguzi wa jana ni pigo kwa chama cha kishoshiliasti tangu katika daraja ya kimkoa mpaka kitaifa.

Manuel Valls alikuwa akutane na rais Francois Hollande leo asubuhi kabla ya rais Hollande kuzungumza na waziri mkuu Jean-Marc Ayrault.

Jean Marc Ayrault ameungama anabeba shemu ya dhamana ya pigo hilo linaloashiria na mengine yanaweza kufuata mfano katika uchaguzi wa bunge la ulaya mwezi May ujao na ule wa baraza la senet ambao unaweza kupibndua wizanio wa nguvu na kuelemea mrengo wa kulia.

Nukhsii inaiandama serikali ya kisoshialiti

Pigo la uchaguzi limechanganyika na ripoti zilizochapishwa leo kuhusu kuongezeka nakisi ya bajeti ya nchi hiyo.Katika wakati ambapo lengo lilikuwa kuipunguza hadi asili mia 4.1 ya pato la ndani kwa mwaka 2013 dhidi ya asili mia 4.9 mwaka 2012,nakisi hiyo imefikia asili mia 4.3.

Bildergalerie Eiffelturm Touristen
Mnara wa Eifel:Kivutio cha watalii mjini ParisPicha: FRANCK FIFE/AFP/Getty Images

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman