1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataalamu wasifia makubaliano ya WTO

Klaus Dahmann9 Desemba 2013

Shirika la biashara duniani WTO limekubaliana juu ya hatua za kuyawezesha masoko ya dunia kuwa huru, hataua ambayo wataalamu wa uchumu wanasema itaboresha uchumi wa dunia, lakini hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa.

https://p.dw.com/p/1AVES
Picha: Reuters/Edgar Su

Mkuu wa WTO Roberto Azavedo alizungumzia juu ya kile alichokiita makubaliano ya kihistoria. Huku akitokwa machozi ya furaha alisema kuwa wameirudisha dunia katika shirika la biashara duniani, na kwamba kwa mara ya kwanza katika historia, WTO imeweza kufanikisha jambo.

"Wanachama wetu walioendelea na wanaoendelea wanatekeleza wajibu wao katika mazungumzo haya, wakisaidia kuja na makubaliano yaliyo katika maslahi yao. Na kwa hivyo nina furaha kusema kwamba, kwa mara ya kwanza katika historia, WTO imefanya kweli," alisema Azavedo baada ya kufikiwa kwa makubaliano hayo.

Mkuu wa WTO Roberto Azavedo.
Mkuu wa WTO Roberto Azavedo.Picha: Reuters

Makubaliano kuchochea ukuaji wa uchumi
Makubaliano yaliyofikiwa na WTO kisiwani Bali yanalenga kushughulikia vikwazo vya kibiashara, hasa urasimu, na kufanya mabadiliko yanayonuiwa kurahisisha biashara duniani.

Kodi za uingizaji bidhaa na ruzuku za kilimo pia vitapunguzwa, kwa sababu vinafanya iwe vigumu kwa mataifa maskini kushindana na mataifa yaliyoendela kiviwanda kutoka barani Ulaya. Jürgen Mattes kutoka taasisi ya utafiti wa kiuchumi nchini Ujerumani, alisema katika mahojiano na DW kwamba hatua hizi zitasaidia kuboresha ukuaji wa uchumi.

Naye makamu wa zamani wa rais wa taasisi ya uchumi wa dunia ya mjini Kiel Rolf Langhammer, alisema katika mahojiano na DW, kwamba jaribio la kuondoa vikwazo vya biashara ya kilimo ni ishara njema.

"Jambo zuri ni kwamba kuna jitihada za kuweka viwango sawa vya forodha duniani kote. Iwapo hilo litawezekan katika mataifa maskini ni suala jengine. Utekelezaji wake unaweza kuchukuwa muda lakini pia msaada upo," alisema Langhammer.

Katika siku za usoni, ushuru wa forodha unaweza kuchukuwa nafasi ya vikwazo vya bishara ya kilimo, na hii inamaanisha kwamba taifa linaweza kuuza nje bila kikomo, lakini kodi za ziada zitakuwa zinatozwa kwa bidhaa zinazodi kikomo cha sasa.

Ujumbe wa India katika Mkutano wa tisa wa WTO ulifanyika kisiwani Bali nchini Indonesia.
Ujumbe wa India katika Mkutano wa tisa wa WTO ulifanyika kisiwani Bali nchini Indonesia.Picha: Reuters/Edgar Su

Hali haikuwa ya matumaini siku ya Alhamisi, baada ya India kusisitiza kwamba inataka ruhusa ya kutoa ruzuku katika mchele na nafaka nyingine kuhakikisha kuwa raia wake maskini zaidi wapatao milioni 800 wanaendelea kupata chakula kwa bei nafuu, suala ambalo liliafikiwa kwa kuiruhusu nchi hiyo kutoa ruzuku ndani ya vikomo vilivyo bayana na chini ya usimamizi wa karibu.

Habari nzuri kwa uchumi wa Ujerumani
Mbali na mataifa maskini, Ujerumani pia itafaidika na makubaliano ya Bali. Mkurugenzi wa biashara ya nje katika baraza la biashara na viwanda la Ujerumani Volker Treier, aliyaelezea makubaliano hayo kama ishara muhimu, na kusema kwamba yanaweza kuuimarisha uchumi wa Ujerumani kwa kuuongezea kiasi cha euro bilioni 60 kwa mwaka.

Ikiingiza zaidi ya asilimia 7 ya mapato yatokanayo na mauzo ya nje duniani, Ujerumani inashika nafasi ya tatu baada ya China na Marekani, na kila moja kati ya nafasi nne za ajira nchini Ujerumani inahusiana na mauzo ya nje.

Mwandishi: Ignatzi Christian
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Daniel Gakuba