1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataliban ni changamoto Afghanistan

30 Mei 2011

Shambulio la kujitolea mhanga nchini Afghanistan na kuenea kwa bakteria za E.coli kulikosababisha hadi vifo vya watu kumi na maelfu wengine kulazwa hospitali ndio mada kuu hii leo magazetini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/RQna
Ein Bundeswehrsoldat beobachtet die Landstrasse bei der Ortschaft Madrassa am Stadtrand von Kunduz in Afghanistan. Aussenminister Guido Westerwelle (FDP) hat im Bundestag einen schrittweisen Abzug deutscher Soldaten aus Afghanistan ab Ende 2011 angekuendigt. In den ersten Provinzen werde die Sicherheitsverantwortung bereits im ersten Halbjahr des kommenden Jahres an die Afghanen uebergeben, sagte der FDP-Politiker am Donnerstag (16.12.10) bei seiner Regierungserklaerung zu "Fortschritten und Herausforderungen in Afghanistan". Ende 2011 werde dann das Bundeswehrkontingent in Afghanistan erstmals reduziert. (zu dapd-Text) Foto: Michael Kappeler/ddp/dapd
Vikosi vya Ujerumani vyasaidia kulinda usalama AfghanistanPicha: AP

Basi tukianza na Afghanistan gazeti la BERLINER ZEITUNG linaandika:

"Hivi sasa Waziri wa Ulinzi, Thomas de Maiziére, akitoa mwito kwa umma kuiunga mkono kwa dhati operesheni ya wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanistan, basi kwanza anapaswa kueleza ukweli wa mambo, yaani vita hivi havishindiki. Na ikiwa hiyo ndio hali halisi, basi kilichobaki ni kuhakikisha kuwa idadi ya wahanga itakuwa ndogo na wanajeshi wanaporejeshwa nyumbani hatua hiyo ichukuliwe kuambatana na masharti yatakayozingatia watu wa Afghanistan na majeshi ya mataifa shirika nchini humo."

Operesheni ya Afghanistan imeshindwa linaandika gazeti la RHEIN-NECKAR, na kuongezea hivi:

"Sasa cha kufanywa ni kujiandaa kuondoka nchini humo kwa njia ambayo itazuia umwagaji mkubwa wa damu. Wakati huo huo, mfumo wa ulinzi uimarishwe, ili usalama wa kudumu wa aina fulani upatikane katika nchi hiyo inayoteseka."

Gazeti la STUTTGART NACHRICHTEN nalo linatoa sura inayovunja moyo. Linasema hivi:

"Hali itazaidi kuwa mbaya nchini Afghanistan. Umwagaji damu uliotokea siku ya Jumamosi ni mfano mmoja tu. Mshambuliaji wa kujitoa mhanga aliwaua watu saba, wakiwemo wanajeshi wawili wa Kijerumani. Na Jenerali wa Kijerumani amejeruhiwa katika shambulio hilo. Tukio hilo limeathiri uongozi wa vikosi na limedhihirisha kuwa Wataliban wana uwezo wa kuendeleza vita vyao vya kigaidi. Mara nyingine tena waasi wamefanikiwa kusababisha wasiwasi miongoni mwa viongozi na polisi nchini humo na kuvilazimisha vikosi vya kimataifa, ISAF, kuufikiria upya mkakati wake."

Kwa upande mwingine, gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG linasema:

"Ule wakati ambapo kila nchi iliachiwa kushughulikia hatima yake, ni hali isiyopo tena. Hii leo nchini Afghanistan, jumuiya ya kimataifa inasaidia kulinda haki na uhuru wa ulimwengu wa magharibi na wa watu wa Afghanistan. Ujumbe huo unatekelezwa na vijana wa Kijerumani wanaokabiliana na hatari ya kifo - bila shaka wanastahili kuheshimiwa."

Sasa tunageukia mada nyingine inayoenedelea kugonga vichwa vya habari nchini Ujerumani- kuenea kwa bakteria za E.coli kulikosababisha vifo vya watu 10 na zaidi ya watu elfu moja kuambukizwa, baadhi yao wakiwa mahututi. Gazeti la VOLKSSTIMME linasema:

" Kilichodhihirika kufuatia maambukizo ya bakteria za E.coli, ni kwamba maendeleo yaliyopatikana kiviwanda katika sekta ya kilimo, miongo hii iliyopita yamesaidia kuondosha njaa, lakini maendeleo hayo yameleta hatari mpya kwa afya ya binadamu. Ionekanavyo, hata udhibiti mkali hautoi kinga. Wakulima wachache wanaweza kudhuru mamilioni ya walaji."

Kwa maoni ya gazeti hilo, katika siku zijazo itakuwa bora kwa wateja kununua mazao yanayotoka kwa wakulima walio nchini mwao.

Mwandishi:Martin,Prema/dpa

Mhariri:Othman,Miraji