1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataliban ni wapiganaji waliobobea

15 Aprili 2010

Mzozo wa madeni ya serikali ya Ugiriki unaoathiri sarafu ya Euro;operesheni ya majeshi ya Ujerumani nchini Afghanistan ni baadhi ya habari zilizotawala safu za mbele katika magazeti ya Ujerumani leo Alkhamisi.

https://p.dw.com/p/Mwqa

Lakini mada inayotufungulia makala yetu inahusika na hatua iliyochukuliwa kupunguza muda wa kufanya kazi badala ya waajiriwa kuachishwa kazi kabisa. Sera hiyo imesaidia soko la ajira laandika gazeti la SCHWÄBISCHE ZEITUNG na kuongezea:

"Ujerumani ilichukua hatua sahihi kuendelea na mpango wa kufupisha saa za kufanya kazi badala ya waajiriwa kuachishwa kazi. Nchi zingine zilizoendelea kiviwanda zinatuonea wivu. Kwani Uingereza, Ufaransa na Marekani idadi ya wakosa ajira imeongezeka sana kwa sababu ya kukosekana hatua kama hiyo. Kwa hivyo wafanyakazi wa Ujerumani wavumilie kufanya kazi saa chache, kwani hatimae watanufaika, hasa makampuni makubwa yatakapoimarisha mauzo yake katika nchi za nje."

Lakini gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG linasema:

"Itakuwa kosa kuisifu sera ya kufupisha muda wa kazi kama kichocheo cha kupunguka idadi ya wasio na ajira. Ujerumani, kinyume na nchi nyingi zingine za Ulaya, idadi ya wasio na ajira haikuongezeka kwa kiwango kikubwa, kwa sababu ya mageuzi yaliyofanywa katika soko la ajira wakati wa uongozi wa serikali ya Schroeder pamoja na hatua za tahadhari zilizochukuliwa na wafanya biashara.Kwani wafanyabiashara hao wamejifunza kuwa anaefukuza wafanyakazi wenye ujuzi wakati wa shida, hatopata haraka hivyo wafanyakazi wazuri,uchumi utakapoimarika."

Gazeti hilo likiendelea linasema:

"Kwa hivi sasa hatua ya kupunguza muda wa kazi haiwezi kuepkwa, lakini serikali ikumbuke kuwa wanaoathirika ni wafanyakazi."

Tukitupia jicho mada nyingine, gazeti la MÜNCHNER MERKUR linasema:

"Taliban sio kundi la wasiokuwa na nidhamu kama watu wanavyofikiria, bali wengi wao ni wapiganaji wa kigeni waliobobea na ambao kifo hakiwashtui. Jambo hilo linajulikana tangu zamani mjini Berlin. Kwanini watu wamenyamaza? Jawabu ni wazi."

Na gazeti la DER NEUE TAGE linaandika:

"Vita" - neno lililokuwa likihofiwa kwa muda mrefu, limeanza kutamkwa serikalini. Lakini wanajeshi walijua tangu zamani hatari ya jukumu lao. Vita ni neno ambalo walioko nyumbani hawapendi kulisikia. Asilia 62 ya umma unataka wanajeshi warejeshwe nyumbani, hayo ni kwa mujibu wa jarida la Der Stern.

Sasa tunatupia jicho mada inayoendelea kugonga vichwa vya habari - Ugiriki na tatizo lake la madeni. Gazeti la NORDWEST ZEITUNG limeandika:

"Ugiriki iliyokumbwa na matatizo ya fedha inaendelea kuathiri thamani ya sarafu ya Euro. Hata mpango uliopendekezwa na Umoja wa Ulaya kuanzisha mfuko maalum wa fedha haukusaidia cho chote. Mpango huo, huenda ukasaidia kuzuia mgogoro wa fedha kwa muda mfupi tu. Hata nchi kama Ureno,Ireland na Italia zinahesabiwa kama nchi zinazoyumba kiuchumi.

Kwa maoni ya NORDWEST ZEITUNG kinachohitajiwa ni marekebisho katika mfumo wa sarafu ya Euro. Kwani hivi sasa, kuambatana na Mkataba wa Maastricht, nchi isiyofuata mwongozo wa kundi linalotumia sarafu ya Euro, haiwezi kufukuzwa.

Mwandishi:Prema Martin/DPA

Mpitiaji:Abdul-Rahman