1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataliban Wafungua Ofisi ya Uwakala Doha

1 Aprili 2013

Amiri wa Qatar, Sheikh Hamad Bin Khalifa al-Thani, amezungumza na Rais Hamad Karzai wa Afghanistan kuhusu kufunguliwa ofisi ya uwakala wa wataliban nchini humo katika kuhimiza juhudi za amani nchini Afghanistan

https://p.dw.com/p/187cq
Amiri wa Qatar Sheikh Hamad bin Khalifa Al-ThaniPicha: picture-alliance/dpa

Kwa mujbu wa shirika rasmi la habari la Qatar, mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na maafisa wa ngazi ya juu wa pande zote mbili, yamemulika uhusiano wa nchi hizo mbili pamoja na "masuala yanayohusiana na masilahi ya pande mbili".

Awali shirika hilo la habari la Qatar halikuzungumzia suala la kufunguliwa, ofisi ya uwakala wa Wataliban katika nchi hiyo ya kifalme - ambalo kusema kweli ndilo lililokuwa chanzo cha ziara iliyoanza Jumamosi na kumalizika jana Jumapili ya Rais Karzai na mawaziri kadhaa wa serikali yake mjini Doha.

Ilikuwa jana usiku tu ndipo shirika rasmi la habari la Qatar lilipotaja kwamba mazungumzo hayo "yalituwama katika suala la makadirio ya amani nchini Afghanistan."

"Tutazungumzia bila ya shaka kuhusu utaratibu wa amani na kufunguliwa ofisi ya uwakala wa wataliban nchini Qatar" alisema hapo awali msemaji wa ofisi ya rais ya Afghanistan Aimal Faizi,salipohojiwa na shirika la habari la Ufaransa-AFP.

Rais Karzai abadilisha msimamo wake

Katika wakati ambapo Qatar imekaribisha fikra ya kufunguliwa ofisi hiyo ya uwakala katika juhudi za kurahisisha juhudi za amani,hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa kuhusu matokeo ya mazungumzo pamoja na rais Karzai.

Mapema mwaka huu,rais wa Afghanistan aliipinga fikra ya kufunguliwa ofisi hiyo ya uwakala wa wataliban nchini Qatar,akihofia serikali yake isije ikajikuta inatengwa katika mazungumzo  kati ya waasi na wawakilishi wa serikali ya Marekani.Fikra hiyo aliibadilisha baadae.

"Ofisi ya uwakala ni mahala ambapo wanamgambo wanaweza kuketi na kuzungumza na serikali ya Afghanistan.Haiwezi kutumika vyengine"Alisisitiza Aimal Faizi.

Wataliban daima wamekuwa wakipinga kuzungumza na rais Karzai,wanaemtuhumu kuwa "kibaraka wa Marekani."

Hoja hizo wamezirejea upya jumamosi iliyopita."Kufunguliwa ofisi ya uwakala wa wataliban hakuhusiani hata kidogo na Karzai.Ni suala linalowahusu wataliban na serikali ya Qatar tu." amesema msemaji wa wataliban-Zabiullah Mudjahid na kuongeza kwamba wawakilishi wao walioko Doha hawatoonana na rais Karzai.

Amani lazma ipatikane

Ehemalige Taliban-Kämpfer
Wapiganaji wa zamani wa Taliban wakisalimisha silaha zao July 14 mwaka 2012 huko HeratPicha: picture-alliance/dpa

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Afghanistan alisema hivi karibuni mazungumzo pamoja na wataliban hayatoanza kabla ya kwanza "wataliban kuvunja uhusiano na Al Qaida na kuachana na ugaidi."

Wataliban wamevunja mazungumzo ya awali ya Doha pamoja na Marekani Marchi mwaka jana kutokana na kila upande kushindwa kukidhi madai ya mwengine.

Lakini miaka chini ya miwili kabla ya kuondolewa sehemu kubwa ya wanajeshi wa jumuia ya kujihami ya NATO,makubaliano ya amani yamekuwa ya lazima ikiwa watu watataka kuiepushia nchi hiyo balaa la kutumbukia upya katika janga la vita vya wenyewe kwa wenyewe kama vile vilivyoripuka kati ya mwaka 1992 hadi 1996.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef