1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataliban wakiri wamefanya shambulio la Lahore

Miraji Othman28 Mei 2009

Shambulio la Lahore limefanywa na Wataliban

https://p.dw.com/p/Hyzd
Waokozi wanatafuta miili ya watu katika shambulio la bomu mjini LahorePicha: AP

Kiongozi wa Wataliban aliye na cheo cha juu huko Pakistan amedai kwamba kundi lake ndilo linalobeba dhamana ya shambulio kubwa lililosababisha vifo vinge mjini Lahore, na akasema kwamba kitendo hicho kilikuwa kulipizia kisasi kwa operesheni zionazofanywa na jeshi la nchi hiyo katika eneo la kaskazini magharibi. Nayo serekali ya Pakistan imesema itatoa zawadi ya Rupia za Kipakistani milioni tano, yaani dola za Kimarekani 62,250, kwa mtu yeyote atakayesababisha kukamatwa shehe mwenye siasa kali, Maulana Fazlullah.


Hakimullah Mehsud, makamo wa mkuu wa Wataliban wa Pakistan, Baitullah Mehsud, ameliambia leo kwa njia ya simu shirika la habari la Associated Press, AP, kwamba shambulio la bunduki na la bomu liloelekezwa kwa majengo ya polisi na makachero mjini Lahore lilihusika moja kwa moja na mashambulio yanayoendeshwa na jeshi la Pakistan katika Bonde la swat. Watu 30 waliuwawa na karibu ya 250 walijeruhiwa katika shambulio lilofanywa jumatano katika mji wa mashariki wa Lahore. Maafisa wa hospitali na wa serekali wanasema polisi 15 na raia 11 waliokuwa karibu na mahala pa tukeo hilo ni miongoni mwa wale waliokufa. Idadi hiyo haiingizi makachero ambao miili yao ilipelekwa katika hospitali ya kijeshi.

Baitullah Mehsud amedai kwamba kundi lake linabeba dhamana ya shambulio la bundiki na mabomu ya kurusha kwa mkono lililofanyiwa shule ya polisi hapo Machi 30. Naye makamo wake, Hakimullah Mehsud, amesema ikiwa serekali ya Pakistan, kwa kushahwishiwa na Marekani, itafanya operesheni zaidi katika Bonde la Swat, basi wao watayalenga zaidi majengo ya serekali. Alisema yeye anawapenda raia wa Pakistan, kwa hivyo anatoa ombi kwao waihame miji yao kwa vile kutakuweko hujuma kubwa zaidi, tena zilizo za hatari zaidi kuliko hujuma za karibuni; na malengo yatakuwa majengo ya serekali. Wapelelezi wa serekali ya Pakistan walisema kwamba katika hujuma ya jumatano walikuweko washambuliaji watatu, ambao walitoka kwenye gari lililopakiwa baruti. Walifyetua risasi na kurusha magrenedi. Mmoja kati ya washambuliaji hao aliuliwa kwa risasi, sekundi chache baadae gari hilo liliripuka na kuwauwa wawili wengine waliobakia.

Operesheni za jeshi la Pakistan zina makusudio ya kuwafyeka Wataliban ambao walisonga mbele na kufika hadi kilomita 100 kutoka mji mkuu wa Islamabad. Japokuwa uasi wa Wataliban hasa umejikita katika mkoa wa kaskazini magharibi, eneo linalopakana na Afghanistan, hata hivyo, kuna makundi kadhaa yalio na makao yao katika mkoa wa Punjab, ambayo yameanzisha mafungamano ya karibu na watu wenye maingiliano na mtandao wa al-Qaida.

Nayo serekali ya Pakistan itampa zawadi ya Rupia za Kipakistan milioni tano, yaani dola 62,250, mtu yeyote atakayesababisha kukamatwa kwa shehe mwenye siasa kali, Maulana Fazlullah, muasisi wa uasi wa Wataliban katika Bonde la Swat. Serekali imechapisha majina ya watu wanaotafutwa, ikiwa wahai au wemekufa, akiwemo msemaji wa Wataliban katika bonde la Swat, Muslim Khan. Tangazo lenye majina hayo lilikuwa na kichwa cha Aya ya Koran, ikisema: msisambaze michafuko katika ardhi. Zawadi itakayotolewa kwa wandani wa Faizullah ni baina ya Rupia milioni moja hadi nne. Tangazo hilo liliuliza: jee watu ambao wamewapotezea wanawake, dada na binti majumba na kuwafanya wasiwe na mwahala pa kuishi katika nchi yao wenyewe wanaweza kuitwa Waislamu na wazalendo wa Pakistan? Lilisema watu hao ni wauwaji wa binadamu na wanastahili adhabu.