1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watatu wakamatwa baada ya shambulizi Jakarta

Admin.WagnerD15 Januari 2016

Polisi nchini Indonesia imesema shambulizi lilofanywa na washambuliaji wa kujitoa muhanga, katikati ya mji mkuu wa nchi hiyo Jakarta, lilifadhiliwa na kundi linalojiita dola la kiisalmu IS.

https://p.dw.com/p/1He6W
Indonesien Bombenanschläge in Jakarta
Picha: Reuters/D. Whiteside

Siku moja baada ya kutokea kwa shambulizi hilo, polisi tayari imeshawakamata watu watatu wanaoshukiwa kuhusika, hali kadhalika waligundua bendera ya kundi la IS kutoka kwa mmoja ya waliojiripua kwa mabomu.

Mkuu wa jeshi la polisi nchini humo,Jenerali Badrodin Haiti, aliwaarifu maripota kwamba shambulizi hilo la siku ya Alhamisi lilifadhiliwa na kundi la IS kupitia, Bahrun Naim, raia wa Indonesia aliyetumikia kifungo cha mwaka mzima gerezani kwa makosa ya kumiliki silaha kinyume na sheria mwaka 2011, na ambaye sasa inasemekana yupo nchini Syria akipigania kundi la IS.

"Nimetembelea eneo la shambulizi na nimekutana na watu wanaofanya kazi ndani ya jengo hilo la biashara, kila kitu kinaonekana kurudi katika hali ya kawaida. Jana nilipowauliza wengi walisema wanahofu sana, lakini sasa kila kitu kimerudi kuwa sawa, na hilo ndio muhimu zaidi," alisema rais wa nchi hiyo Joko Widodo.

Aidha jana, kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter wafuasi wa kundi la IS pia walisambaza ujumbe unaodai kuwa wamehusika na shambulizi hilo. Ikithibitishwa kwamba kundi la IS limehusika na shambulizi hilo, basi vikosi vya usalama nchini humo vitakabiliwa na changamoto kubwa sana.

Kundi hilo lenye misimamo mikali ya kidini linadhibiti maeneo makubwa nchini Syria na Iraq, na dhamira yake ya kuunda miliki ya Khalifa au dola la kiislamu imevutia zaidi ya wapiganaji 30,000 kutoka nchi mbalimbali duniani, wakiwamo Waindonesia na Wamalay.

Der indonesische Präsident Joko Widodo am Anschlagsort in Jakarta
Rais wa Indonesia Joko Widodo akitembelea eneo la shambuliziPicha: Reuters/W. Putro/Antara Foto

Wengi waliouawa ni washambuliaji

Watu saba ndio waliouawa kutokana na shambulizi hilo la jana, watano kati yao wakiwa ni washambuliaji wenyewe. Hata hivyo, hili ni mara ya kwanza kwa kundi la IS kulilenga taifa hilo lenye idadi kubwa ya waislamu duniani. Na tukio hili linaashiria kuanza kwa mashambulizi ya aina mpya, katika nchi iliyozoea mashambulizi madogomadogo ambayo kawaida huwalenga polisi.

Wakuu wa polisi nchini humo walitakiwa kuwa katika hali ya tahadhari, na balozi kadhaa mjini Jakarta zilifungwa kwa siku nzima. halikadhalika usalama uliimarishwa katika kisiwa cha Bali ambacho ni maarufu miongoni mwa watalii wanaotoka Australia na nchi nyengine za bara la Asia.

Mchambuzi wa masuala ya ugaidi,Taufik Andri, amesema ingawa shambulizi hilo lilimalizika haraka na zaidi liliwaumiza washambuliaji wenyewe, lengo lao lilikuwa ni kuonyesha uwepo wao na uwezo wao nchini humo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape/rtre

Mhariri: Daniel Gakuba