1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watendaji Facebook, Twitter, Google kutoa ushahidi seneti

Iddi Ssessanga
1 Agosti 2018

Watendaji wakuu wa kampuni za Facebook, Twitter na Google watatoa ushahidi katika kamati ya upelelezi ya baraza la seneti Septemba 5, amesema naibu mwenyekit wa kamati hiyo Seneta Mark Warner kutoka chama cha Democratic.

https://p.dw.com/p/32Ssn
Symbolbild Soziale Netze
Picha: picture-alliance/dpa/Heimken

"Tutawakaribisha watendaji wa juu kutoka Facebook, Twitter na ndiyo, Google katika kikao Septemba 5. Kusikiliza mipango waliyonayo, kuwabana kufanya zaidi, na kushirikiana katika kushughulikia tatizo hilo," Warner alisema wakati wa kikao kinachochunguza juhudi za mataifa ya nje kushawishi uchaguzi wa Marekani kupitia mitandao ya kijamii.

"Ingawa ushahidi ambao kamati imeuona hadi sasa unaashiria kwamba kampuni hizo za mitandao ya kijamii - hasa Facebook, Instagram, Twitter, Google na Youtube - nado zina kazi kubwa ya kufanya," alisema Warner.

Kamati hiyo imekuwa ikiangalia suala hilo kwa miezi kadhaa, lakini wasiwasi uliongezeka siku ya Jumanne, wakati Facebook iliposema iligundua kampeni mpya inayoratibiwa kushawishi kampeni ili kuwapotosha watumiaji wake na kupanda mbegu za mgawanyiko miongoni mwa wapiga kura kuelekea uchaguzi wa kati mwa muhula nchini Marekani.

Kikao hicho, ambacho kilihusisha ushahidi kutoka kwa wataalamu wa tekonolojia na usalama wa mtandaoni, kilipangwa muda mrefu kabla ya tangazo la Facebook.

Mark Warner
Naibu mwenyekiti wa kamati ya upelelezi ya bunge la Seneti nchini Marekani, Seneta Mark Warner.Picha: Getty Images

"Wakati ni suala la kushtua kwamba watu wa nje walitumia mitandao ya kijamii na njia za mawasiliano ambazo ni muhimu sana katika maisha yetu katika juhudi za kuingilia msingi wa demokrasia yetu, kinachotatiza hata zaidi ni kwamba bado jambo hilo linaendelea hadi hii leo," alisema Seneta Richard Burr, mwenyekit wa kamati hiyo kutoka chama cha Republican, wakati wa ufunguzi wa kikao hicho.

Warner alihoji kwamba wahalifu wa mtandaoni waliokamatwa "walikuwa tu wale wasiojimudu," na kusema alikuwa na wasiwasi kwamba serikali ya Marekani haijapanga vizuri kubaini au kukabiliana na operesheni za ushawishi kwenye mitandao ya kijamii.

Facebook ilisema Jumanne kuwa ilikuwa imeondoa kurasa 32 na akaunti za bandia kutoka Facebook na Instagram, kama sehemu ya juhudi za kupambana na uingiliaji wa nje katika uchaguzi wa Marekani.

Kampuni hiyo haikutoa taarifa kuhusu vyanzo vya taarifa hizo za upotoshaji. Lakini wajumbe wa bunge walioarifiwa kuhusu suala hilo walisema mbinu ya kampeni ya ushawishi ilionyesha ushiriki wa serikali ya Urusi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Josephat Charo