1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto wa kupanga kutoka Afrika ,je ni matumaini mema?

Sekione Kitojo11 Oktoba 2010

Watoto wanaochukuliwa na watu wengine kuwalea katika nchi za nje kunatokana na sababu mbali mbali, mara nyingi ikiwa ni umasikini na kutokuwa na mzazi hata mmoja.

https://p.dw.com/p/Pb3S
Waethiopia wakisubiri msaada wa chakula katika mji wa Wadla, umasikini husababisha wazazi kukubali kuwatoa watoto wao kwa wazazi wa kupanga.Picha: AP

Watoto wanaochukuliwa na watu wengine kuwalea katika nchi za nje kutokana na sababu mbali mbali, mara nyingi hujikuta katika utamaduni na mazingira mapya kabiasa ya kimaisha.

Ghafla watoto hujikuta wakiwa katika utamaduni mpya kabisa, bila ya kufahamu lugha ama kutambua kile kilichowatokea, ama hata kujua kwamba watawaona tena wazazi wao. Huu ni mustakabali wa baadhi ya watoto wa Afrika. Wakikabiliwa na umasikini uliokithiri, wazazi wanashindwa hata kuwalea watoto wao. Kwa jina la kuwapa mapenzi pamoja na hali bora ya maisha ya baadaye wanawatoa kwa wazazi wa kambo. Ripoti ya Jane Ayeko inasomwa studioni na Sekione Kitojo.

Picha zilikuwa kila mahali. Mwanamuziki maarufu wa Marekani Madonna akiwa na mtoto wa kiume kutoka Afrika . Lakini kupangwa kwa mtoto huyo kulizusha hali ya tahadhari kimataifa na ukosoaji wakati taarifa hizo ziliposambaa kuwa mtoto huyo hakuna yatima. Hata hivyo, Madonna alisisitiza kuwa anampa mtoto huyo hali bora ya maisha ya baadaye. Wazazi wengi kutoka mataifa ya magharibi wanafikiri kama anavyofikiri Madonna. Kwa mujibu wa shirika linalojulikana kama Okoa watoto, kupanga watoto kumeongezeka katika muda wa miaka ya hivi karibuni ambapo wazazi kutoka nchi za magharibi wakikimbilia hususan katika bara la Afrika na Asia kutafuta watoto. Katika bara la Afrika , Ethiopia imekuwa na idadi kubwa ya watoto ambao wanapelekwa nchini Marekani, Australia pamoja na mataifa mengine ya Ulaya.

Susanne Christensen ni mkurugenzi wa okoa watoto nchini Ethiopia. Amewaona wazazi wakishawishiwa kuwatoa watoto wao.

Hawajui sheria, hawajui kile kinachowatokea watoto wao na mara nyingi wako katika hali mbaya ambapo huwa tayari kupokea fedha na kisha wanafikiri kuwa kila kitu kitakuwa safi.

Katika nchi ambayo haina msaada wa marupurupu ya kuwasaidia watoto kwa familia zenye mahitaji, ama hata fedha za ulezi kwa wale ambao wanawahudumia watoto yatima, ama watoto walioachwa bila wazazi, kuwatoa watoto kwa ajili ya kupanga ni chaguo la haraka na rahisi. Kwa mujibu wa sheria za Ethiopia, mtoto mwenye mzazi mmoja hawezi kutolewa kwa ajili ya kupangwa. Lakini hata hivyo hiyo haizuwii utaratibu huu, anasema Susanne Christensen.

Kuna mashirika ya kusaidia watoto wa kupanga ambayo yanatumia mtindo wa kuwadanganya wazazi ili kuwatoa watoto wao kwa ajili ya kupanga. Bila kutambua kile wanachokifanya na kuambiwa kuwa watoto wao watarejea hivi karibuni.

Wakati huo huo kuna fedha nyingi katika biashara hii ambayo huenda katika nyakati fulani inafungua njia za rushwa. Kwa hiyo nadhani ni sekta yenye utata sana.

Kwa upande mwingine wa bara hilo, Ghana ina kiwango cha chini cha watoto wa kupangwa licha ya kuwa kisheria mtoto anaweza kupangwa, na si tu mayatima. Mchungaji Emmanuel Kwesi Nkurumah ni mkurugenzi wa wakfu wa shirika la huruma kwa binadamu, shirika ambalo linasaidia watoto wenye shida nchini Ghana. Haoni tatizo lolote dhidi ya kupanga watoto, kwani mtoto anapochukuliwa na wazazi wengine nje ya Ghana, atajifunza utamaduni mwingine ambako elimu ni nzuri zaidi na atapata malezi mazuri zaidi.

Mwandishi : Jane Ayeko / ZR / Sekione Kitojo.

Mhariri : Abdul-Rahman