1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto wanaendelea kutumiwa jeshini Afrika

12 Februari 2013

Kwa mara ya 11 walimwengu wanaikumbuka "siku ya kimataifa ya mkono mwekundu" wakiitikia wito wa mashirika ya haki za binaadamu na mashirika yanayopigania masilahi ya watoto, kupinga kutumiwa watoto vitani.

https://p.dw.com/p/17cfu
Mtoto wa miaka 12 aliyewahi kupigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra LeonePicha: picture-alliance/dpa

Sudan, Sudan kusini, Somalia, Chad, hizo ni nchi chache tu ambako watoto walilazimika kutumika katika vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka ya hivi karibuni. Katika Afrika ya Magharibi, vita vya Mali ndivyo vinavyozusha wasi wasi kwa sasa. Shirika linalopigania haki za binaadam la Human Rights Watch linaamini makundi ya itikadi kali ya dini ya Kiislam yamewalazimisha maamia ya watoto,wawatumikie na kuteremka vitani. Corinne Dufka anaongoza tawi la Human Rights Watch Afrika magharibi. Katika mazungumzo pamoja na wahusika katika eneo la kaskazini la Mali, ameweza kujionea hali halisi ya mambo namna ilivyo:Anasema" yadhihirika kana kwamba wazee wengi wamewakabidhi watoto makundi ya itikadi kali ya dini ya kiislam baada ya kupokea fedha. Wafuasi wa itikadi wamekuwa wakiwasajili watoto katika vijiji fulani tu - kule ambako wakaazi wanafuata nadharia kali ya dini ya Kiislam.

Watoto wameonekana Gao

Joseph Kony Rebellenführer LRA Uganda Archivbild
Joseph Kony anaongoza kundi la waasi la Uganda LRAPicha: Stuart Price/AFP/Getty Images

Katika baadhi ya visa, wanamgambo wa kiislam wamewatanguliza watoto makusudi mbele katika uwanja wa mapigano-anasema bibi Dufka.Mashahidi wamewaaona watoto karibu na kambi za wanamgambo kaskazini mashariki ya mji wa Gao-muda mfupi kabla ya jeshi la wanaanga la Ufaransa kuanza hujuma zao.Hatima ya watoto hao mpaka leo haijulikani,anasema mtaalam huyo wa masuala ya Afrika magharibi.

Hata kama watoto wameweza kukimbia, lakini walichokishuhudia kitawaandama kwa muda wote wa maisha yao. Hilo limedhihirika kutokana na hali ya watoto waliowahi zamani kutumiwa vitani. Watoto kama hao sio tu wanasumbuliwa kisaikolojia,mara nyingi wanakuwa pia hawana elimu wala mafunzo ya kazi. Hali hiyo amekumbana nayo Eric Mongo Malolo wa jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Amebuni shirika analoliita "Afya" na kuwahudumia watoto katika mkoa wa Ituri, kaskazini mashariki ya nchi hiyo-eneo lililoshuhudia muongo mzima wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.Eric Mongo Malolo anahisi hata hivyo kusaidia watoto tu haitoshi:

Jamii inahitaji pia kuelimishwa

Demokratische Republik Kongo Wahl Wahlen 2011 Kindersoldaten Kindersoldat
Mtoto anaetmiwa katika vita katika eneo la mashariki la jamhuri ya kidemokrasi ya KongoPicha: picture alliance/dpa

"Jamii wanatuangalia kana kwamba tunawasaidia wale waliofanya maovu.Kwa hivyo tunalazimika pia kushirikiana na jamii ili watoto hawa wapate kutambuliwa ,kusaidiwa na kujumuishwa katika jamii."Anasema mwanzilishi wa shirika la "Afya"

Mongo Malolo na shirika lake "Afya" anawahudumia watoto 520,tangu mradi wake ulipoanza miaka mitatau iliyopita.Shirika hilo ni sehemu ya Mtandao unaojiita "Haki na Amani".Unagharimiwa na fuko maalum linalosimamiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu lililoundwa mwaka 2002.

Mwandishi: Philipp Sandner/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Mohammed Khelef