1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto wazidi kuteketezwa Syria

Admin.WagnerD15 Julai 2013

Majeshi ya serikali ya Syria yamevishambulia vijiji vinavyodhibitiwa na waasi katika mkoa wa kaskazini wa Idlib kwa maroketi, mizinga na ndege, na kuua watu wasiopungua 29, wakiwemo watoto sita.

https://p.dw.com/p/197vl
Watoto wakipanga foreni ya chakula cha futari.
Watoto wakipanga foreni ya chakula cha futari.Picha: Reuters

Mashambulizi hayo yamefanyika wakati mjumbe maalumu wa Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa kuhusu watoto, akisafiri kwenda Syria kuzungumzia ongezeko la mauaji ya watoto katika mgogoro huo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.Picha: imago/Xinhua

Assad yajivunia nguvu mpya

Baada ya kupata nguvu katika miezi ya hivi karibuni, vikosi vya rais Bashar al-Assad hivi sasa vimezidisha mashambulizi dhidi ya waasi katika maeneo mbalimbali, ukiwemo mkoa wa Idlib, ulioyoko katika mpaka wa Syria na Uturuki. Vikosi vya serikali kwa sasa vinadhibiti mji mkuu wa mkoa huo Idlib, wakati brigedi kadhaa za waasi zinadhibiti maeneo ya nje ya mji huo.

Shirika la uangalizi wa haki za binaadamu la Syria lenye makao yake mjini London Uingereza limesema mashambulizi ya usiku wa kuamkia leo yalilenga vijiji vitano karibu na mji wa Idlib, ambapo wanawake wanane na watoto sita walikuwa miongoni mwa watu 29 waliouawa. Shirika hilo ambalo linakusanya taarifa zake kutoka kwa mtandao wa wanaharakti walioko ndani ya Syria, limesema kuwa shambulio baya zaidi lilitokea katika kijiji cha Maghra, ambapo kombora liliangukia nyumba na kuua watu kumi na watatu.

Katikati mwa Syria, bomu la kutegwa kwenye gari liliripuka nje ya makao makuu ya polisi katika mji wa Deir Atiyeh, uliyoko kilomita 80 kutoka mji mkuu Damascus, na kuua watu 13, wakiwemo maafisa 10 wa polisi, na mtoto mmoja. Hakukuwa na kundi lolote lililodai kuhusika na shambulio hilo, lakini makundi yaliyo na mafungamano na matandao wa Al-qaeda yamekuwa yakizilenga taasisi za serikali, majengo ya kiuslama na vikosi vya serikali kwa kutumia mabomu ya kutega kwenye magari na mashambulizi ya kujitoa mhanga.

Wapiganaji wa Jeshi Huru la Syria, FSA wakiwa mkoani Idlib.
Wapiganaji wa Jeshi Huru la Syria, FSA wakiwa mkoani Idlib.Picha: Reuters

Mjumbe wa Ban Ki-Moom ziarani Syria

Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto, Leila Zerrougui yuko nchini Syria kwa siku tatu ambapo atafanya mazungumzo na maafisa wa serikali, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali, kama sehemu ya ziara itakayomfikisha pia nchi jirani za Jordan, Iraq, Lebanon na Uturuki, ambazo ndiyo zimewapokea kwa wingi, wakimbizi kutoka Syria.

Kwa mujibu wa shirika la uangalizi wa haki za binaadamu, zaidi wa watu laki moja wamekwishauawa tangu kuanza kwa uasi dhidi ya rais Assad mwezi Machi mwaka 2011, na zaidi ya 5,000 kati ya hao ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 16.

Siku ya Jumapili, shirika hilo lilionya kuwa mamia ya familia zilikuwa zimekwama katika wilaya ya Qaboon mjini Damascus, ambako mapigano makali yalikuwa yakiendela, kwa sababu walenga shabaha wa utawala wa Assad waliwekwa nje ya mji huo. Hadi sasa hakuna taarifa zilizotolea kuhusiana na masaibu yao.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, ape
Mhariri: Saum Yusuf