1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 100 wadaiwa kufa Libya

25 Machi 2011

Sauti za miripuko mikubwa ya makombora kutoka angani imesikika tena leo (25.03.2011), Kaskazini mwa mji wa Tripoli, ikiwa sehemu ya mashambulizi ya majeshi ya Muungano kuzuwia ndege kuruka katika anga ya Libya.

https://p.dw.com/p/10hI2
Majeshi ya Libya yakikagua kifusi cha jengo baada ya mashambulizi
Majeshi ya Libya yakikagua kifusi cha jengo baada ya mashambuliziPicha: AP

Akielezea tukio hilo pasipo ufafanuzi wa kina, msemaji wa jeshi la Libya amedai raia na wanajeshi kadhaa wameripuliwa na makombora hayo kutoka ndege za kivita.

Mashambulizi haya ya leo yamefanyika muda mfupi baada ya Umoja wa Kujihami wa NATO kutangaza kuanza kushiriki rasmi katika operesheni ya kimataifa nchini Libya.

Wakati majeshi ya Muungano yakiendeleza mashambulizi, msemaji wa serikali ya Libya, Moussa Ibrahim, ameonya kuhusu makombora yaliyoporomoshwa jana, ambayo yalilenga jengo la kituo cha taifa cha televisheni pamoja na radio ya nchi hiyo.

Amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati kwa kukemea kitendo hicho cha kuangamiza taasisi hiyo muhimu ya umma wa Walibya.

Raia miongoni mwa wahanga

Waombolezaji wakisubiri kuzika miili ya jamaa zao, baada ya mashambulizi
Waombolezaji wakisubiri kuzika miili ya jamaa zao, baada ya mashambuliziPicha: AP

Taarifa za maafisa wengine wa Libya pamoja na wahudumu wa hospitali kadhaa, zinasema raia, wakiwemo wanawake, ni miongoni mwa waliouwawa katika mashambulizi yaliyofanyika katika maeneo ya Tripoli.

Serikali ya nchi hiyo imesema kwamba, mpaka jana idadi ya watu waliokufa kutokana na mshambulio hayo imefikia 100, huku ikilalamikia nchi za Magharibi kuingia vitani kwa niaba ya waasi.

Maafisa kwa upande wa vikosi vya Muungano wamekanusha kuhusika na kifo chochote kutokana na operesheni zao ambazo leo hii zimeingia siku ya saba.

Hapo jana (24.03.2011) mfanyakazi wa chumba cha maiti katika hospitali kubwa mjini Tripoli, Ahmed Hussein, aliwaonesha waandishi wa habari maiti 15 za wanaodaiwa kufa kutokana na mashambulizi hayo.

Mfanyakazi huyo aliwaambia waandishi hao wa habari kwamba maiti hizo ni kwa tukio la siku hiyo tu na kwamba bado kuna miripuko mingine katika makazi ya wanajeshi imetokea.

Miili ya watu hao ilikuwa imelazwa katika vigari vya kubebea maiti, zikiwa zimefunikwa na mashuka mazito ya rangi tofauti tofauti.

Serikali ya Libya imetilia mkazo kauli yake ya kwamba majeshi ya Muungano yanauwa kwa kutolea mfano mashambulio ya mji wa Tajura uliyopo mashariki mwa Tripoli.

Hata hivyo, waasi nao wanasema vifo vilivyotokea huko ni vya watu wao.

Kwa ujumla, bado majeshi ya Gaddafi yanasonga mbele katika mashambulio ya ardhini, ingawa inaonekana nguvu zake zimedhoofishwa na vikosi vya anga baada ya kuyashambulia makao ya uongozi wa jeshi lake anga, kama ilivyoelezwa na Uingereza hapo awali.

Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Libya, Khalid Kaim, amesema hali ilivyo katika mji wa Misrata, ambao ni wa tatu kwa ukubwa nchini humo, ni ngumu sana.

"Maisha hayajarejea katika hali ya kawaida Misrata kwa sababu bado kuna watu wanadungua watu kwa risasi pamoja na mashambulio ya anga kutoka majeshi ya Muungano." Amesema Kaim.

Huko katika mji wa mashariki wa Benghazi, waasi wanaendelea na mazoezi ya kijeshi, huku Baraza lao likisema lina wapiganaji takribani 1,000 walio katika uwanja wa vita.

Mwandishi: Sudi Mnette/DPAE/Reuters
Mhariri: Miraji Othman