1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 140 wauawa Yemen katika vita vilivyopamba moto

7 Aprili 2015

Mapigano makali kati ya waasi wa Houthi na wapiganaji watiifu kwa utawala wa Yemen yamesababisha vifo vya watu 140 huku shirika la msalaba mwekundu likishindwa kufikisha misaada ya kibinadamu kwa waathiriwa.

https://p.dw.com/p/1F3Oo
Picha: picture-alliance/AP Photo

Wafanyakazi wa kutoa misaada wameonya kuwa hali inazidi kuwa mbaya katika taifa hilo masikini la kiarabu ambako Saudi Arabia na washirika wake wamekuwa wakifanya mashambulizi ya kijeshi ya angani kwa siku kumi na tatu sasa dhidi ya waasi wa Houthi.

Maafisa nchini humo wamesema mapigano makali yameripotiwa katika mji wa kusini mwa nchi hiyo wa Aden anakotoka Rais wa Yemen Abderabbo Mansour Hadi ambaye ametorokea Saudi Arabia.

Watu 53 ambao ni thuluthi moja ya waliouawa katika kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita, waliuawa wakati waasi wa Houthi walipojaribu kuidhibiti bandari moja mjini Aden.

Waasi 19 wa Houthi na wapiganaji 15 wa makundi ya wapiganaji wanaomuunga mkono Hadi wameuawa usiku wa kuamkia leo katika mji wa Daleh kaskazini mwa Adeb na watu wengine saba wameuawa katika jimbo la kusini mwa Yemen la Abyan.

Mji wa Aden waathirika zaidi

Wapiganaji wanaomuunga mkono Hadi wanaidhibiti kambi ya Abyan ya kikosi cha wanajeshi walio watiifu kwa Rais wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh anayeshutumiwa kuwaunga mkono waasi wa Houthi.

Waasi wa Houthi mjini Aden
Waasi wa Houthi mjini AdenPicha: picture-alliance/AP Photo/Wael Qubady

Hadi ambaye anatambuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa kiongozi halali wa Yemen, alitorokea Aden mwezi Februari baada ya wahouthi kuuteka mji mkuu Sanaa na kuchukua madaraka. Baadaye mwezi uliopita alikimbilia Saudi Arabia baada ya waasi hao kuanza kuusogelea mji wa Aden na kuichochea Saudi Arabia na nchi nyingine za kisunni kuanzisha kampeini ya kijeshi dhidi ya waasi hao.

Vita hivyo vinavyozidi kulisambaratisha taifa hilo vimegawanyika katika makundi mengi yakiwemo waasi wa Houthi, wapiganaji watiifu kwa Hadi, vikosi vya wanajeshi watiifu kwa Saleh, waasi wa kutoka kusini mwa Yemen wanaotaka kujitenga kwa eneo hilo, makundi ya wapiganaji wa kisunni na wanamgambo wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda.

Shirika la msalaba mwekundu limetoa wito kwa mapigano kusitishwa ili liweze kuwasilisha misaada ya kibinadamu inayohitajika kwa dharura kwa waathiriwa ikiwemo tani 48 za vifaa vya matibabu ili kutoa huduma kwa kiasi ya watu 3,000 waliojeruhiwa.

Misaada inahitajika kwa dharura

Hali ni mbaya zaidi mjini Aden ambako baadhi ya maeneo yamekuwa bila ya umeme na maji kwa siku kadhaa sasa. Shirika la msalaba mwekundu limesema limeshindwa kupeleka misaada mjini humo kwa sababu ya matatizo ya kiufundi na bado halijapata hakikisho la kiusalama kutoka kwa pande zinazopigana.

Raia wa Yemen wakichakura vifusi
Raia wa Yemen wakichakura vifusiPicha: picture alliance/abaca

Hapo jana India iliwaondoa raia wake 450 kutoka nchini Yemen,China iliwaondoa raia wake 100, Jordan imewaondoa raia 300 tangu mzozo kuanza Yemen na Ufaransa pia imewaondoa raia wake 63 nchi hizo zote zikitumia meli kuwasafirisha raia wake.

Pakistan imesema imeombwa na Saudi Arabia kujiunga na kampeni ya kijeshi kwa kutuma majeshi yake, suala ambalo bunge la nchi hiyo linafanya kikao maalum ili kufikia uamuzi katika siku chache zijazo.

Iran ambayo imekanusha kuwaunga mkono waasi wa Houthi imelaani vikali kuingiliwa kijeshi kwa Yemen na nchi zinazoongozwa na Saudi Arabia huku waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarifa akitarajiwa kuzuru Islamabad hapo kesho kuujadili mzozo huo.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/Ap

Mhariri: Gakuba Daniel