1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 17 wauwawa kwenye shambulizi la bomu nchini Sri Lanka

29 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CUPK

Waasi wa Tamil Tigers wamefanya shambulizi la bomu katika ghala moja la serikali ya Sri Lanka kwenye kitongoji cha mji mkuu Colombo, Nugegoda.

Duru za jeshi la Sri Lanka zinasema watu 17 wameuwawa katika shambulizi hilo nadra la kuwalenga raia, wakati bomu mfano wa kifurushi lilipolipuka kwenye mlango wa kuingia ndani ya eneo la maduka katikati mwa kitongoji cha Nugegoda. Watu wengine 33 walijeruhiwa katika mlipuko huo.

Serikali ya Sri Lanka imelilaumu kundi la waasi la Tamil Tigers kwa hujuma hiyo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amelilaani vikali shambulizi hilo la bomu na kutoa mwito machafuko yakome nchini Sri Lanka.

Shambulizi hilo limefanywa baada ya mshambulizi wa kike kujilipua karibu na ofisi ya waziri wa ustawi wa jamii, Douglas Devenad wa kabila la Tamil na kumuua katibu wake. Waziri huyo alinusurika lakini watu wengine wawili walijeruhiwa.