1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Darfur: Watu 18 wauawa kwenye mapigano ya kikabila

Zainab Aziz Mhariri Mohammed Khelef
5 Aprili 2021

Watu wengine 54 waliojeruhiwa wanapatiwa matibabu kwenye hospitali ya mafunzo ya Al-Janeina iliyopo kwenye jimbo hilo. Kamati ya madaktari imetoa taarifa hii.

https://p.dw.com/p/3rbH6
Anja Niedrighaus Preis 2016, Foto von Adriane Ohanesian
Picha: A. Ohanesian

Watu wapatao 18 wameuawa kutokana na mapigano ya kikabila katika jimbo la Darfur nchini Sudan.

Mapigano hayo yaliyotokea kwenye mji wa El-Jeneina ni kati ya mengi yaliyokuwa yanazuka hivi karibuni katika jimbo la Darfur. Tangu kutiwa saini mkataba wa amani mwaka uliopita na tangu kuondoka kwa majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa mnamo mwezi Januari, watu wapatao 129 wameshauawa licha ya vikosi vya usalama kuimarishwa katika mji huo.

Mapigano hayo ya hivi karibuni ni kati ya watu wa kabila la Masalit na makabila ya Kiarabu yalipamba moto kuanzia siku ya Ijumaa (Aprili 4). Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa shirika la habari la Reuters, silaha nzito ikiwa pamoja na roketi za kurushia maguruneti zilitumika katika mapigano hayo. Moshi mwingi uliweza kuonekana hadi kwenye maeneo ya jirani.

Wakimbizi wa ndani katika kambi moja wapo ya wakimbizi kwenye jimbo la Darfur
Wakimbizi wa ndani katika kambi moja wapo ya wakimbizi kwenye jimbo la DarfurPicha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Adam Regal, msemaji wa asasi inayosaidia katika shughuli za kuendesha kambi za wakimbizi katika mji wa Darfur, alielezea juu ya guruneti lililopiga kwenye kambi ya wakimbizi katika mji wa Jenena siku ya Jumatatu (Aprili 5), ambalo lilisababisha moto ulioteketeza nyumba kadhaa za wakimbizi hao. Alisema hali ni ngumu sana na mbaya.

Mnamo mwezi Oktoba, mkataba wa amani ulitiwa saini baina ya serikali ya mpito ya Sudan na makundi ya waasi yaliyopambana na rais wa hapo awali wa Sudan, Omar al Bashir, aliyetimuliwa madarakani na wanajeshi wake.

Hata hivyo, mashambulio yaliyokuwa yanafanywa na makabila ya Kiarabu yaliyokuwa yanapatiwa silaha na utawala wa al-Bashir yamekuwa yanaongezeka. Kutokana na hali hiyo mapigano yamepamba moto katika siku za hivi karibuni katika jimbo la Darfur.

Wakimbizi wanawake katika kambi ya Zam Zam kwenye jimbo la Darfur
Wakimbizi wanawake katika kambi ya Zam Zam kwenye jimbo la DarfurPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Prinsloo

Licha ya serikali ya Sudan kusema kwamba ingelikuwa na uwezo wa kuwalinda wananchi wake, raia wa nchi hiyo wameeleza kuwa wana wasiwasi. Mwaka uliopita Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika waliondoa majeshi yao ya kulinda amani baada ya kuwepo nchini Sudan kwa muda wa miaka 13. 

Wanajeshi hao walikwenda baada ya mapigano kuzuka kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2003 na kusababisha vifo vya watu wapatao 300,000 na wengine zaidi ya milioni 2.5 waligeuka kuwa wakimbizi wa ndani.

Mgogoro huo ulipungua kasi katika miaka ya hivi karibuni lakini mapigano ya hapa na pale yamekuwa yanaendelea ambapo watu wa makabila mbalimbali wamekuwa wanapigania maji na rasilimali zingine.

Vyanzo:AFP/RTRE/AP