1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 200 wafa maji Sudan kusini

14 Januari 2014

Kiasi ya watu 200 kutoka Sudan Kusini wamefariki leo Jumanne katika ajali ya feri katika Mto Nile wakati wakikimbia mapigano katika mji wa Malakal.

https://p.dw.com/p/1AqB0
Südsudan Kämpfe Flüchtlinge in Bor
Wananchi wa Sudan kusini wakikimbia mapiganoPicha: Reuters

Taarifa zinazopatikana kutoka Sudan Kusini zinasema watu kati ya 200 na 300, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto wamekufa maji katika ajali hiyo ya feri. Chombo hicho kilikuwa na watu wengi kuliko uwezo wake, amesema msemaji wa jeshi Philip Aguer.

Ameongeza kuwa wote wamefariki. Walikuwa wakikimbia mapigano ambayo yalizuka tena katika mji wa Malakal.

Mapigano yanaendelea

Mapigano yameendelea katika maeneo mbali mbali leo(14.01.2014) katika Sudan ya kusini . Mapigano makali yameripotiwa kutokea katika mji wa Malakal, mji mkuu wa jimbo linalotoa mafuta kwa wingi la Upper Nile, wakati waasi walipofanya mashambulizi mapya kuukamata mji huo, ambao umekuwa ukibadilisha udhibiti mara mbili kati ya waasi na jeshi la serikali tangu mzozo huo kuanza Desemba 15 mwaka jana nchini Sudan Kusini.

Konflikt im Südsudan Regierungssoldaten 25.12.2013
Wanajeshi wa serikali wakipambana na waasiPicha: Samir Bol/AFP/Getty Images

Kuna mapigano mapya ndani na nje ya mji wa Malakal, amesema mkuu wa misaada ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Sudan kusini Toby Lanzer, na kuongeza kuwa kituo cha jeshi la kulinda amani limefurika karibu mara mbili ya idadi ya watu wanaohitaji hifadhi, kutoka 10,000 hadi 19,000.

Jeshi limeripoti kutokea mapigano makali kusini mwa mji wa Bor, wakati serikali ilitaka kuudhibiti tena mji wa huo kutoka kwa waasi, mji mkubwa pekee ambao bado uko katika udhibiti wa waasi.

Hata hivyo amekataa madai ya waasi kuwa wamekamata tena bandari ya Mongola katika mto Nile, mji iliyopo kati ya mji wa Bor na mji mkuu Juba.

Pia amethibitisha kuwa kumekuwa na mapigano makali kusini mwa mji mkuu, katika mji wa Rajaf jana.

Malakal in Südsudan
Mji wa MalakalPicha: Reuters

Miili yatapakaa barabarani

Wakati huo huo miili kadha ya watu , ikiwa ni pamoja na miili ambayo imeharibika imetapakaa barabarani kutoka uwanja wa ndege hadi katika mji mkuu wa jimbo linalotoa mafuta kwa wingi nchini Sudan kusini la Unity. Nyumba na majengo mbali mbali pamoja na maduka yamechomwa moto ama kuharibiwa na kumekuwa na uporaji mkubwa, huku magari yaliyoharibiwa na kuchomwa moto yakifuka moshi.

Matokeo ya vita mjini Bentiu na uharibifu uliotokea katika taifa hilo jipya duniani yanaonekana wazi, wakati jeshi la serikali likiendelea kupambana na wanajeshi ambao walilitumikia jeshi hilo mwezi mmoja uliopita, ambao hivi sasa wanaitwa waasi.

Hayo yakiendelea viongozi wa Japan na Ethiopia wamezitaka pande zinazopigana nchini Sudan Kusini kutia saini makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yamesababisha maelfu ya watu kuuwawa.

"Tumekubaliana kuwa usitishaji wa uhasama nchini Sudan Kusini na mapatano ya kitaifa ni muhimu sana," waziri mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn, amesema katika mkutano wa pamoja na waandishi habari akiwa na mwenzake wa Japan, Shinzo Abe.

Äthiopien Ministerpräsident Hailemariam Desalegn
Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam DesalegnPicha: Getty Images

Matamshi hayo yamekuja huku mazungumzo ya amani mjini Addis Ababa kati ya pande hasimu nchini Sudan kusini yakiendelea mjini Addis Ababa. Ethiopia na Japan zimesema zinataka uthabiti nchini Sudan Kusini, nchi ambayo imepata uhuru mwaka 2011 kutoka Sudan.

Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe/ape

Mhariri: Mohammed Khelef