1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 39 wauawa mkesha wa Mwaka Mpya Istanbul

Mohammed Khelef
1 Januari 2017

Watu wapatao 39 wameuawa kufuatia mashambulizi ya "kigaidi" mjini Istanbul, baada ya mtu aliyevalia kama Santa Klaus kuingia kwenye klabu ya usiku ambako watu walikuwa wakishangiria kuingia kwa Mwaka Mpya.

https://p.dw.com/p/2V6Lz
Türkei Istanbul Anschlag auf Nachtclub Polizei
Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Sandal

Polisi wanaendelea na msako wa kuwatafuta waliohusika na mashambulizi hayo, wakati Rais Recep Tayyip Erdogan amesema shambulizi hilo lililenga kusababisha machafuko na kuhujumu amani, lakini Uturuki haitakata tamaa. Awali mtu huyo mwenye silaha pia alimuua polisi mmoja na raia aliyekuwa nje ya klabu ya Reina, moja ya maeneo ya kifahari, katika mji mkuu huo wa Uturuki.

"Kwa bahati mbaya, raia wetu 35 wamepoteza maisha yao. Mmoja alikuwa afisa wa polisi. Watu 40 wanapatiwa matibabu mahospitalini," alisema gavana wa Istanbul, Vasip Sahin, akiwa eneo la tukio.

"Mshambuliaji huo - kikatili na bila huruma - aliwalenga watu wasiokuwa na hatia waliokwenda kusherehekea Mwaka Mpya na kufurahi," alisema gavana huyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Dogan, washambuliaji walikuwa wawili na wote walivalia mavazi ya Santa Klaus, au Father Krismasi. 

Türkei Istanbul - Sanitäter transportieren verletzte nach Angriff auf Nachtclub
Watu wengine walijeruhiwa katika shambulizi hiloPicha: Reuters/Stringer

Picha za televisheni zilionesha watu waliokusanyika kwenye mkesha huo wa Mwaka Mpya wakitoka kwenye klabu iliyoshambuliwa wakiwa na nguo zao za faragha, huku wakiwa wameghumiwa.

Kwa mujibu wa meya huyo, mashambulizi yalianza saa 7:15 usiku kwa majira ya Istanbul, muda mchache baada ya washangiriaji hao kuuona Mwaka Mpya.

Fadhaa na wasiwasi katikati ya sherehe

"Kilichotokea leo ni mashambulizi ya kigaidi," alisema gavana huyo.

Hata hivyo, gavana huyo hakubainisha endapo mshambuliaji naye aliuawa au endapo alikuwa na wenzake wengine.

Watu kadhaa walijirusha kwenye Mto Bosphorus kutokana na fadhaa na juhudi za kuwaokoa ziliendelea kwa masaa kadhaa, kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha NTV. 

Shirika la habari la Digan liliripoti kwamba baadhi ya mashahidi walidai kuwa washambuliaji walikuwa "wakizungumza Kiarabu", huku mtangazaji wa kituo cha NTV akisema kuwa maafisa wa polisi walikuwa wakiendelea na msako kwenye klabu hiyo ya usiku.

Picha za televisheni zilionesha maafisa hao wa polisi wakilitanda eneo hilo. Kwa mujibu wa shirika la habari la Dogan, kulikuwa na watu 700 waliokuwa wakisherehekea kuanza kwa mwaka 2017 kwenye klabu hiyo wakati inashambuliwa.

Klabu hiyo iko kwenye wilaya ya Ortakoy, moja ya maeneo ya wenye kipato katika mji mkuu huo, na huwa linatembelewa na watu wenye fedha zao tu. 

Tayyip Erdogan
Rais Erdogan amesema waliohusika wanasakwaPicha: Reuters/Presidential Palace/M. Cetinmuhurdar

Uturuki yaendelea kushambuliwa

Uturuki imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara, ambapo serikali imekuwa ikiwalaumu wapiganaji wa Kikurdi na wa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu. 

Mnamo tarehe 10 Disemba, watu 44 waliuawa kwenye mashambulizi mawili ya mabomu mjini Istanbul baada ya mechi ya mpira wa miguu katika eneo la Besiktas, upande wa pili wa Mto Bosphorus. Mashambulizi hayo, ambayo yalililenga basi la polisi, yalidaiwa kufanywa na wanamgambo wa kundi la Kurdistan Freedom Falcons (TAK) linalotambuliwa kama tawi la msimamo mkali la PKK.

Wiki moja baadaye, wanajeshi 14 wa Uturuki waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa kwenye mashambulizi ya kujitoa muhanga ambayo nayo yalitajwa kufanywa na TAK yakiwalenga wanajeshi ambao hawakuwa kazini. 

"Hakuna mashambulizi ya kigaidi yatakayoharibu umoja wetu, au kuondoa udugu wetu, au kudhoofisha vita vya Uturuki dhidi ya ugaidi," aliandia Waziri wa Sheria Bekir Bozdag kwenye mtandao wa Twitter.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Isaac Gamba