1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 4 wauwa na wengine 14 kujeruhiwa katika mapigano Basra

Kalyango Siraj25 Machi 2008

Amri ya kutotembea usiku imetangazwa Basra

https://p.dw.com/p/DTwA
Polisi wa Iraqi wakijihami mjini Basra, 550 kilometers kusini-mashariki mwa Baghdad, Iraq, Jumanne, March 25, 2008. Vikosi vya Iraq vimepambana dhidi ya wanamgambo wa Kishia wa Muqtada al- Sadr katika operesheni ya kuyanyanganya silaha makundi haramu katika mji huoPicha: AP

Mapigano makali yamelipuka katika mji wa kusini mwa Iraq wa Basra kati ya vikosi vya usalama vya Iraq dhidi ya jeshi la Mahdi ambalo ni kundi la mgambo la kiongozi wa kishia katika eneo hilo Muqtadar al-Sadr.

Kwa mujibu wa mwandhishi wa habari wa shrika la kifaransa la AFP alieshuhudia mapigano hayo anasema kuwa,milio ya risasi za rasharasha pamoja na ya mizinga ilianza kusikika punde tu baada ya vikosi vya usalama kuingia katika kitongoji cha Al-Tamiyah ambacho ni kitovu cha jeshi la wanamgambo wa kundi la Moqtada al-Sadr mapema alfajiri, saa za Basra.

Baadae mapigano yalisambaa katika mitaa mingine ya karibu katika mji wa Basra ambao uko umbali wa kilomita 550 kusini mwa mji mkuu wa Baghdad.

Polisi imehakikisha kuwa operesheni inaendelea dhidi ya wanamgambo wa jeshi la Mahdi mjini Basra huku kundi la Sadr likisema liko tayari kujadilia usitishwaji wa mapigano.

Waziri mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki, yuko mjini Basra kuongoza operesheni hiyo.

Duru za kijeshi katika mji huo zinasema kuwa jeshi la Uingereza haliusiki katika operesheni hiyo ambayo inasemekana imechukuliwa ili kupokonya silaha kutoka kwa makundi haramu katika mji huo.

Maafisa wa hospitali kuu katika mji huo,wanasema kuwa watu kadhaa ambao wamejeruhiwa wameanza kuletwa katika hospitali hiyo,ingawa kulikuwa hakujatolewa ripoti za kuwepo na watu waliouawa wakati huo.Hata hivyo taarifa za hivi punde zinasema kuwa watu wanne ndio wameuwa hadi sasa na wengine 14 ndio wamejulikana kuwa wamejeruhiwa.

Msemaji wa ofisi ya kundi la Sadr ya mjini Basra,Harith al-Athari,ameliambia shirika la habari la AFP kuwa wafuasi wa kundi lao walikuwa tayari kumaliza mvutano uliopo.

Mapigano hayo yanatokea siku moja baada ya waziri mkuu wa nchi hiyo kuanza ziara yake huko na pia baada ya tangazo la jumatatu la kamanda wa jeshi la Iraq anaehusika na usalama kusini mwa Iraq ,Generali Mohan al-Furayji kuonya kuwa operesheni ya kiusalama itafuata katika mkoa mzima wa Basra.

Generali Mohan,alitangaza amri ya kutotoka nje usiku kati ya saa nne za usiku hadi kumi na mbili alfajiri katika mji wa Basra.

Kuanzia kesho,jumatano,barabara zote kutoka maeneo jirani kuelekea mji wa Basra zitafungwa kwa mda wakati wa jioni hadi ijumaa.

Shule za upili mkiwemo vyuo vikuu, nazo zimefungwa kuanzia leo jumanne hadi alhamisi.

Mfanya biashara mmoja katika mji wa Basra amesema kuwa wanajeshi wengi waliwekwa katika barabara za mji huo usiku wa kuamkia leo na watu wengi hawakutoka majumbani mwao leo.

Mkoa wa Basra, wenye utajiri wa mafuta,ulikabidhiwa kwa utawala wa Iraq kutoka kwa jeshi la Uingereza mwezi disemba.