1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 80 wauawa karibu na balozi za kigeni Afghanistan

Mohammed Khelef
31 Mei 2017

Watu wapatao 80 wameuwawa na wengine zaidi ya 300 kujeruhiwa baada ya bomu lililotegwa kwenye gari kuripuka katika mtaa wenye ofisi za balozi nyingi mjini Kabul.

https://p.dw.com/p/2dt2D
Afghanistan Explosion in Kabul
Picha: Reuters/O. Sobhani

Mabaki ya miili ya watu ilitapakaa na moshi mkubwa ulionekana ukitoka kutoka katika eneo hilo ambalo lina balozi mbali mbali za mataifa ya kigeni.

Balozi za Ufaransa na Ujerumani ni miongoni mwa zilizoathirika na mashambulizi hayo, ambapo mlinzi wa Kiafghani kwenye ubalozi wa Ujerumani anatajwa kuwa mmoja wa waliouawa.

Katika taarifa yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, aliyalaani vikali mashambulizi hayo, lakini pia alisisitiza kuendelea kwa nchi yake kuisaidia Afghanistan kurejesha amani na kujijenga upya.

Ingawa hakuna kundi lililodai kuhusika na mashambulizi hayo wala kufahamika kwa lengo lake, lakini kutokea kwake kunaashiria kuwa bado hali ya usalama ni mbaya nchini  Afghanistan, ambako majeshi ya nchi hiyo yanakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa wapiganaji wa itikadi kali na pia kukimbiwa na maafisa wake kadhaa.