1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 9 wafa katika mashambulio ya mabomu Jakarta, Indonesia

Kabogo Grace Patricia17 Julai 2009

Rais wa Indonesia, alaani vikali mashambulio hayo yaliyotokea katika hoteli mbili za kifahari mjini Jakarta.

https://p.dw.com/p/IrU2
Mmoja wa watuhumiwa wa ugaidi, Abu Dujana wa kundi la Jemaah Islamiyah, linalotuhumiwa kuhusika na mashambulio ya Bali, 2002 Indonesia.Picha: AP

Rais wa Indonesia, Susilo Bambang Yudhoyono, amesema taarifa za usalama zimeeleza kwamba kulikuwa na mpango wa kuchochea ghasia nchini humo, ukiwemo mpango wa kumuua yeye mwenyewe na kuwataka maafisa wa usalama kuchunguza endapo mashambulio ya mabomu yaliyotokea leo katika hoteli mbili za kifahari mjini Jakarta, ni sehemu ya mpango huo.

Rais Yudhoyono, amelaani vikali mashambulio hayo ya kigaidi yameyotokea katika hoteli ya JW Marriott na hoteli nyingine ya karibu Ritz-Carlton, na kusababisha vifo vya watu 9 na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa. Raia wa kigeni 18, ni miongoni mwa watu waliouawa na kujeruhiwa. Aidha, Rais Yudhoyono amesema ana uhakika kuwa waliohusika na mashambulio hayo ya kigaidi watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Mkuu wa Polisi wa Jakarta, amesema kuwa waliohusika na mashambulio hayo ya mabomu ni wateja waliokuwa katika hoteli ya Marriott. Aidha, bomu jingine ambalo lilikuwa bado halijalipuliwa limepatikana katika ghorofa ya 18 katika hoteli ya Marriott.

Mashambulio hayo yamefanyika siku chache baada ya uchaguzi wa rais uliofanyika Julai 9, mwaka huu, ambapo Yudhoyono alishinda na kufanikiwa kuiongoza nchi hiyo katika kipindi cha pili cha miaka mitano, ingawa matokeo ya mwisho bado hayajathibitishwa. Yudhoyono amekuwa akisifiwa katika juhudi za kuweka hali ya usalama nchini kwake, baada ya mashambulio kadhaa yanayodaiwa kufanywa na kundi la Jemaah Islamiyah, tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, amelaani mashambulio hayo ya mjini Jakarta na kuendelea kusisitiza kuwa tishio la ugaidi bado lipo kwa kiasi kikubwa. Bibi Clinton amesema ofisi yake inafanya mipango ya kuwasaidia raia wa Marekani waliojeruhiwa katika mashambulio hayo. Amesema Marekani iko tayari kutoa msaada kwa Indonesia, iwapo nchi hiyo itahitaji msaada wake. Ameongeza kuwa hakuna njia nyingine zaidi ya kukabiliana na vitisho hivyo vya kigaidi, na hiyo itafanyika kwa ushirikiano wa pamoja wa nchi zinazotaka kuwa na hali ya utulivu na amani hapo baadaye.

Kwa upande wake Umoja wa Ulaya nao umelaani vikali mashambulio hayo ya Jakarta na kusema kuwa inaungana na Serikali ya Indonesia katika kupiga vita ugaidi. Taarifa iliyotolewa na Rais wa Umoja wa Ulaya kutoka Sweden, ambayo ndiyo rais wa umoja huo kwa sasa imeeleza kuwa umoja huo unasikitika kutokea kwa mashambulio hayo na kusababisha vifo hivyo na majeruhi.

Nchi nyingine inayoungana na Marekani na Umoja wa Ulaya kulaani mashambulio hayo ya Jakarta, ni Ufaransa, ambayo imesema kuwa iko tayari kutoa ushirikiano kwa waathirika wa mashambulio hayo pamoja na kwa serikali ya Indonesia. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imesema kuwa Ufaransa iko upande wa Indonesia, ambayo ni mshirika wake mkuu katika nchi za Bara la Asia, ambayo inapiga vita ugaidi.

Hii ni mara ya pili kwa hoteli ya Marriott kushambuliwa ambapo Agosti 5, mwaka 2003 yalifanyika mashambulio mengine na kusababisha vifo vya watu 12 na wengine 150, kujeruhiwa.

Mwandishi:Grace Patricia Kabogo (APE/DPAE/AFPE/RTRE)

Mhariri: Miraji Othman