1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu kadha wauawa kwenye shambulizi la hoteli katika mji wa Peshawar nchini Pakistan.

10 Juni 2009

Wanamgambo wa Taliban wametishia kundesha mashambulizi ya kulipiza kisasi harakati za jeshi la Pakistan katika bonde la Swat.

https://p.dw.com/p/I6jy
Hoteli ya Pearl Continental iliyoshambuliwa nchini Pakistan.Picha: picture-alliance/ dpa

Maafisa nchini Pakistan wanaendelea na uchunguzi wa kutaka kubaini waliohusika kwenye shambulizi kwenye hoteli mjini Peshawar lililosababisha vifo vya watu kumi na moja hapo jana Jumanne, wakiwemo wafanyakazi wawili wa umoja wa mataifa waliokuwa wakiisaidia pakistan kutoa huduma kwa wakimbizi wa mapigano katika ya jeshi la Pakistan na wanamgambo wa Taliban .

Karibu washambuliaji watatu wa kujitoa mhanga waliwafyatulia risasi walinzi kabla ya kuingia katika hoteli ya Pearl Continental katika mji wa Peshawar, hoteli inayotembelea na raia wa kigeni pamoja na wapakistan walio na uwezo wa kifedha.

Watu 70 walijeruhiwa kwenye shambulizi hilo ambalo lilitokuea baada ya viongozi wa wanamgambo wa Taliban kutishia kuwa, wataendesha mashambulizi makubwa katika miji mikuu nchini pakistan kulilpiza kisasi harakati zinaoendeshwa na jeshi la pakistan dhidi ya wanagmabo hao.

Camera za usalama zilionyesha washambuliaji hao wakiwa kwenye magari mawili huku mlinzi mmoja wa hoteli hiyo akianguka baada ya kupigwa risasi. Magari hayo kisha yaliingia katika eneo la hoteli na kulipuka

Wanamgambo wa Taliban wamekuwa wakiendesha mashambulizi katika miji kadha nchini Pakistan tangu jeshi la pakistan lianzishe oparesheni mwezi Aprili, ya kuwavurusha wanamgambo wa Taliban kutoka bonde la Swat na kutoka maeneo ya kaskazini magharibi mwa Pakistan.

Hadi leoe miili ya watu saba imepatikana lakini hata hivyo miili ya watu zaidi pamoja na ya washambuliaji bado haijapatikana kutoka kwa hoteli hiyo iliyoharibiwa.

Anschlag in Pakistan auf Luxushotel
Watu waliojeruhiwa katika shambulizi la jana.Picha: AP

Mlipuko huo uliharibu kabisa vioo vya hoteli hiyo na kusababisha baadhi ya kuta zake kuporomoka.Polisi walisema kuwa bomu lililotumika kwenye shambulizi hilo lilikuwa na uzito wa kilio 500, sawa na uzito wa bomu lililotumika katika shambulizi lilitokea katika hoteli ya Marriot mjini Islamabad mwezi Septemba mwaka uliopita ambapo watu 55 waliuawa.

Hakuna yeyote aliyedai kuhusika na shambulizi hilo lakini hata hivyo wanamgambo wa Taliban wamekuwa wakionya juu la kulipiza kisasi harakati za kijeshi, na huenda sasa wanatumia mbinu mpya ya wanagmabo waliojihami ambao huwasaidia washambuliaji wa kujitoa mhanga.

Kuna matarajio kuwa huenda sasa jeshi la pakistan likalenga ngome zingine za wanamgambo kama ile ya kusini mwa Waziristan iliyo katika eneo lililo kwenye mapaka na Afghanistan baada ya oparesheni ya Swat kumalizika.

Ndege za jeshi la pakistan mapema leo ziliendesha mashambulizi katika eneo la Bannu, wilaya ambayo ni kiingilio cha eneo Waziristan. Afisa mmoja wa kijeshi alisema kuwa wanamgambo kadha waliuawa au kujeruhiwa.

Eneo la Wazistan linatajwa kama makao salama ya wanamgambo wa Taliban, wanaondesha harakati zao nchini Afghanistan na maficho ya kundi la al Qaeda, wanaopanga kutekeleza mashambuulizi katika nchi za magharibi.

Jeshi linasema kuwa limefanikiwa katika harataki zake katika bonde la swat hata kama bado linakabiliwa na upinzani wa hapa na pale.Linasema kuwa hadi sasa wanamgambo 1300 wameuawa pamoja na wanajeshi 105, hata kama bado hakuna idadi kamili iliyotolewa.

Mwandishi :Jason Nyakundi/RTR

Mhariri :Mohammed Abdul Rahman