1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bidhaa muhimu huenda zikakosekana Aleppo

Mjahida9 Agosti 2016

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa zaidi ya watu milioni mbili kaskazini mwa Syria wapo katika hatari ya kuzingirwa upya.

https://p.dw.com/p/1JeX3
Syrien Aleppo Kämpfe
Mmoja wa mwanachama wa kundi la wanamgambo akivishambulia vikosi vya serikali mjini AleppoPicha: picture alliance/AA/B. el Halebi

Katika taarifa yake hapo jana, mkuu wa Umoja huo anayeshughulikia masuala ya kibinaadamu nchini Syria, Yacoub El Hillo, pamoja na mratibu wa eneo hilo, Kevin Kennedy, wameomba mapigano yasimamishwe ili kuwepo nafasi ya kupeleka misaada katika maeneo yanayoathirika na vita.

Katika taarifa hiyo pia watu zaidi ya milioni mbili wanasemekana kuishi na hofu ya kuzingirwa wakiwemo watu takriban 275,000 waliokwama Mashariki mwa Aleppo.

Mapigano yanayoendelea mjini humo yameripotiwa kusababisha vifo vya raia 130, tangu mwishoni mwa mwezu Julai na kuharibu vibaya majengo kama hospitali, kliniki pamoja na mitandao ya umeme na maji. Umoja wa Mataifa Hata hivyo umesema uko tayari kuwasaidia wakaazi wa Alepo.

Syrien Aleppo zerstörte Fahrzeuge und Trümmer eines Hauses
Baadhi ya uharibifu mjini AleppoPicha: picture-alliance/AA/Alm Aldeen Al Sabbagh

Umoja huo unahitaji mapigano yasitishwe kabisa au yasimamishwe kwa masaa 48 kila wiki ili kutoa nafasi ya msaada kufikishiwa mamilioni ya watu wanaouhitaji pamoja na kujaza bidhaa kama chakula na dawa ambazo zinahofiwa kupungua kwa kiwango kikubwa.

Mapigano mjini humo yalishamiri mwezi Juni mwaka huu wakati vikosi vya serikali vilipofunga barabara ya Castello ambayo ndio ya mwisho inayoingia katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi. Pande zote mbili zinazohasimiana zina njia zake maalum zinazotumia kufikisha chakula na mahitaji mengine mjini humo, lakini njia hizo bado sio salama kwa matumizi ya raia.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lalaumiwa kwa kushindwa kuchukua hatua Syria

Huku hayo yakiarifiwa wataalamu wameelezea picha za kuogofya za mashambulizi ya mabomu katika maeneo tofauti mjini Aleppo, mashambulizi dhidi ya hospitali, matumizi ya silaha zenye sumu na mateso ya watu yanayoendelea katika mji huo uliozingirwa huku wakisema ni aibu kwa jamii ya Kimataifa kutochukua hatua katika mkutano wa Baraza la usalama uliofanyika hapo jana na uliyoandaliwa na Marekani.

Daktari Zaher Shaloul, daktari Mmarekani aliye na asili ya Syria, amesema hospitali zimekuwa zikishambuliwa mjini Aleppo na watu wanaendelea kufa kutokana na hali ambayo inaweza kutibika kwa kukosekana madawa na vifaa vengine ya afya.

USA New York Sicherheitsrat der Vereinten Nationen über Libyen
Baraza la usalama la Umoja wa MataifaPicha: picture alliance/ZUMA Press/L. Muzi

Shaloul aliyetembelea hospitali moja mjini Aleppo mwezi Julai amesema alimuuliza muhudumu mmoja nini alichokitaka kutoka Umoja wa Mataifa, akamjibu kwamba alichokitaka ni usadizi wa kumhamisha mtoto aliye na umri wa miaka 10 kutoka hospitalini humo ambaye huenda akafariki kutokana na ukosefu wa madawa.

Kwa upande wakebalozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power amelitolea wito Baraza la Usalama la Umoja huo kutuma ujumbe wa pamoja uliyo wazi kuwa mizingiro inapaswa kumalizika na kwamba hakuna sababu au uhalali wa kuwakosesha watu wasio na hatia mahitaji yao muhimu.

Aidha zaidi ya watu 290,000 wameuwawa tangu mapigano yalipoanza nchini Syria miaka mitano iliyopita.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters/Ap

Mhariri: Mohammed Khelef