1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu saba wakamatwa kuhusiana na mashambulizi Uingereza

Maja Dreyer2 Julai 2007

Uchunguzi wa mashambulizi ya kigaidi yasiofaulu nchini Uingereza katika uwanja wa ndege wa Glasgow na katikati ya mji wa London unaendelea. Hadi sasa watuhumiwa saba wamekamatwa. Wakati huo huo, nchi nyingine pia zinajitayarisha kujikinga dhidi ya mashambulizi ya kigaidi.

https://p.dw.com/p/CHBm
Polisi wakishika doria eneo kulikopatikana mojawapo ya gari lililokuwa limetegwa bomu
Polisi wakishika doria eneo kulikopatikana mojawapo ya gari lililokuwa limetegwa bomuPicha: AP

Kulingana na taarifa zilizotolewa na polisi, watuhumiwa wote si Waingereza. Maafisa wa Jordan walisema mmoja kati ya waliokamatwa ni daktari wa Jordan wenye umri wa miaka 27, aliye na asili ya Kipalestinia. Polisi wa Scotland imesema washukiwa wawili wanaoaminika kuhusika katika mashambulio ya uwanja wa ndege wa Glasgow wamefika Uingereza hivi karibuni tu wakitafuta kazi. Mwanzoni kulikuwa na tuhuma ya kwamba washambulizi hao ni Waislamu wa asili ya kigeni waliozaliwa Uingereza kama wale wanaoaminika walifanya mashambulizi ya kujitoa muhanga katika basi na treni mjini London, Julai saba, miaka miwili iliyopita ambapo watu 52 waliuawa.

Kwa mujibu wa kamanda wa kitengo cha polisi cha Scotland Yard kinachopambana na ugaidi, Peter Clarke, habari zinazopatikana juu ya magaidi watuhumiwa zinabadilika kila saa: “Nina uhahika kwamba katika siku na wiki zijazo tutafahamu kikamilifu mbinu zinazotumiwa na magaidi, jinsi wanavyopanga mashambulio yao na mtandao wao.”

Waziri mpya wa mambo ya ndani wa Uingereza, Bi Jacqui Smith, leo asubuhi alisisitiza kwamba kutofaulu mashambulizi haya si kwa bahati tu, bali ni kutokana na uangalifu mkuwba wa raia na polisi wa Uingereza.

Wakati huo huo, waziri mwenzake wa Ujerumani, Bw. Wolfgang Schäuble, pamoja na wanasiasa wengine wanazungumzia hali ya usalama nchini Ujerumani wakiwa na wasiwasi kuwa mashambulizi ya aina hiyo yanaweza kulenga pia nchi hiyo. Kansela Angela Merkel anataka jeshi la Ujerumani liruhusiwe kutumika ndani ya nchi. Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya masuala ya ndani wa Ujerumani hakuna tishio la kigaidi dhidi ya Ujerumani.

Wanasiasa wengine walidai ulinzi wa kamera za video ambao unatumika sana nchini Uingereza, uongezwe hapa Ujerumani. Waziri wa mambo ya ndani, Bw. Schäuble anauunga mkono mwito huu akiwa na hoja nyingine: “Ulinzi kwa kamera za video ni chombo kinachoweza kufaa. Lakini pia tunahitaji sheria ambayo itaiwezesha polisi kuchunguza mawasiliano ya simu, simu za mkononi na kompyuta. Kwani magaida kabla ya kufanya mashambulizi, lazima wawasiliane. Ikiwa tunajua wanapanga nini, tutaweza kuyazuia mashambulizi hayo.”

Mwenyekiti wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, José Barroso, alitoa mwito kwa nchi wanachama wa Umoja huu kushirikiana zaidi katika vita dhidi ya ugaidi.

Baada ya ripoti kujulikana kwamba kundi la kigaidi la Al Qaida linapanga shambulizi kubwa nchini Marekani mwaka huu, waziri wa usalama wa ndani, Bw. Michael Chertoff, aliipuuza ripoti hiyo: “Kiwango cha tishio katika usafiri wa anga tayari ni wa tahadhari ya wastani wa juu, na katika sehemu nyingine ni katika kiwango cha wastani. Kwa sasa hatuoni sababu ya kuongeza kiwango hicho.”

Idara husika za Uingereza zilisema kuna uwezekano kuwa washambulizi wa matukio ya hivi punde nchini humo wana mahusiano fulani na kundi la Al Qaida.