1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wauwawa katika mapigano mapya Somalia

21 Machi 2007

Mapigano makali yamezuka mjini Mogadishu nchini Somalia na takriban watu14 wameuwawa.

https://p.dw.com/p/CHHo

Raia wenye hasira walionekana wakiichoma miili ya wanajeshi wawili ambao waliuwawa katika mapigano hayo huku wakiuburura mwili wa mwanajeshi mmoja na kukumbushia visa vilivyowakumba wanajeshi wa Marekani baada ya mpango wa amani wa umoja wa mataifa nchini Somalia kushindwa mnamo mwanzoni mwa miaka ya 90.

Mashambulio mazito huko kusini mwa mji wa Mogadishu yamesababisha vifo vya askari sita na raia wanane baada ya wapinzani kufyatua risasi kuelekea makao makuu ya wizara ya ulinzi ambako ni kambi ya majeshi ya Ethiopia yanayoilinda serikali ya mpito ya Somalia.

Mamia ya raia katika mji wa jirani wa Baruwa walisherehekea huku wakipiga mayowe ya kulaani majeshi ya Ethiopia na wanajeshi watiifu kwa serikali ya mpito ya rais Abdillahi Yusuf.

Mapigano hayo yalikuwa ya ghafla kwa raia wengi ambao walitaharukishwa na milio ya risasi.

Watu watatu waliuwawa baada ya milipuko ya silaha kupenya hadi ndani ya nyumba yao.

Mkaazi mmoja wa kijiji cha Shukri, Mohamed Ali Shekhe amesema kuwa ameshuhudia vifo vya askari watatu wa serikali katika kambi ya kijeshi ya Hilweyne.

Ripoti kutoka kwenye hospitali tatu za mjini Mogadishu zimesema kuwa zimeorodhesha takriban vifo saba na majeruhi 36 mchana wa leo.

Dahir Mohamed Mohamud Dhere wa hospitali kuu ya mkoa ya Medina amesema kuwa wanatarajia idadi ya majeruhi kuongezeka.

Hadi sasa hospitali hiyo ya Medina ina majeruhi 36 wakiwemo raia na wapiganaji wa pande zote mbili.

Kundi la waasi la Popular Resistance Movement limedai kuwa linalengwa kimakusudi na serikali ya mpito ya Somalia tangu operesheni hiyo ilipoanza siku ya jumatano.

Balozi wa Somalia nchini Kenya Mohamed Ali Nur ametetea hatua ya serikali yake, amesema kuwa hatua hiyo inalenga kusimamisha mashambulio dhidi ya serikali hiyo ya mpito ya Somalia.

Mapigano hayo kati ya wanajeshi wa Ethiopia wakishirikiana na wanajeshi wa Somalia dhidi ya wapinzani wanaodhaniwa kuwa ni wapiganaji wa kiislamu, yalianza siku moja tu baada ya wanajeshi wa kulinda amani wa umoja wa Afrika walipojizatiti katika maeneo ya pwani ya mji mkuu wa Mogadishu.

Kundi la askari 8000 wa umoja wa nchi za Afrika linatarajiwa kukisaidia kikosi cha serikali ya mpito ya Somalia kuidhibiti nchi hiyo.