1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wawili washitakiwa kwa mauaji ya Nemtsov

Mohammed Khelef9 Machi 2015

Washukiwa wawili wa mauaji ya mkosoaji wa serikali ya Urusi, Boris Nemtsov, walifikishwa mahakamani na mmoja wao ni afisa mkubwa wa zamani katika idara ya polisi katika mkoa wa Chechenya.

https://p.dw.com/p/1EnUv
Zaur Dadayev akiwa kwenye kizimba cha mahakama mjini Moscow.
Zaur Dadayev akiwa kwenye kizimba cha mahakama mjini Moscow.Picha: Reuters/T. Makeyeva

Washukiwa hao wawili ni miongoni mwa Wachechenya watano waliokuwa wamefikishwa kwenye chumba cha mahakama mjini Moscow hapo jana, wakiwa wamezibwa nyuso zao kwa vitambaa, huku mikono yao ikifungwa kwa nyuma.

Picha za televisheni zinaowanesha wanaume hao wakiwa wamesimama kwenye vizimba vya chuma huku wapiga picha wa televisheni wakichukua picha zao.

Jaji aliyesimamia kesi hiyo, Natalia Mushnikova, alisema "kuhusika kwa Zaur Dadayev kunathibitishwa na kukiri kwake mwenyewe pamoja na ushahidi uliokusanywa." Dadayev aliwahi kuwa naibu kamanda wa polisi mkoani Chechenya, na kiongozi wa mkoa huo ambaye ni mshirika mkubwa wa Rais Vladimir Putin, Ramzan Kadyrov, amemuelezea Dadayev kama "Muislamu mchamungu aliyekasirishwa na katuni za Mtume Muhammad (S.A.W) katika jarida la dhihaka la Charlie Hebdo nchini Ufaransa.

Boris Nemtsov, aliyekuwa akifuata siasa za kiliberali, aliunga mkono wachoraji wa makatuni kwenye jarida hilo baada ya watu 12 kuuawa pale ofisi za Charlie Hebdo jijini Paris, Ufaransa, zilipovamiwa na watu wenye silaha mwezi Januari mwaka huu.

Uhusiano kati ya mauaji na siasa kali

Wapepelezi nchini Urusi walisema wiki iliyopita kwamba wanachunguza uwezekano kwamba Waislamu wenye siasa kali ndio waliomuua Nemtsov.

Polisi wakimpeleka Zaur Dadayev mahakamani.
Polisi wakimpeleka Zaur Dadayev mahakamani.Picha: Reuters/T. Makeyeva

Kadyrov alimuelezea Dadayev kama "mzalendo wa kweli wa Urusi" ambaye alikuwa amepata medali kadhaa kwa ushujaa wake, lakini hivi karibuni alijiuzulu nyadhifa zake kwenye wizara ya mambo ya ndani kwa sababu ambazo hazikufahamika.

Kumekuwa na mikasa huko nyuma, ambapo waajiriwa wa vyombo vya usalama nchini Urusi wameshitakiwa baada ya kuvujisha taarifa za makundi ya uhalifu wa kupangwa.

Mtu mwengine aliyefunguliwa mashitaka pamoja na Dadayev ni Anzor Gubashev, huku wengine watatu waliofikishwa mahakamani wakiwa ni kaka yake, Shagid Gubashev, Ramzan Bakhayev na Tamerlan Eskerkhanov. Jaji Mushnikova aliamuru wote watano kuendelea kubakia kizuizini.

Upinzani wapinga

Hata hivyo, makundi ya upinzani nchini Urusi yanatilia mashaka taarifa za kukiri kwa Dadayev kuhusika na mauaji hayo ya Nemtsov. Kiongozi wa upinzani Ilya Yashin ameliambia shirika la habari la Urusi kwamba hajui ikiwa wanaoshikiliwa ndio kweli waliofanya makosa.

Mwandishi wa Deutsche Welle mjini Moscow anasema vyama vya upinzani, wafuasi na washirika wao, wanataka uchunguzi wa kina na huru ufanyike juu ya mauaji hayo.

Washirika hao wa Nemtsov, aliyewahi pia kuwa naibu waziri mkuu wa Urusi, wanasema Ikulu ya Kremlin inajipanga kujinufaisha na mauaji hayo kisiasa, ikiwa tayari Rais Putin ameshatoa kauli ya kuyalaani na kuahidi kuchukuwa hatua.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo