1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wazimbabwe bado wasubiri matokeo ya uchaguzi

Charo, Josephat1 Aprili 2008

Polsi waimarisha usalama huku hali ya wasiwasi ikizidi

https://p.dw.com/p/DY9N
Wafuasi wa chama tawala cha ZANU-PF wakishangilia ushindi wa mmoja wa wagombea mjini HararePicha: AP

Hali ya wasiwasi imeendelea kuongezeka nchini Zimbabwe huku Wazimbabwe wakisubiri kutangaziwa kiongozi mpya. Shinikizo linazidi kutaka matokeo kamili ya uchaguzi uliofanyika Jumamosi iliyopita yatolewe haraka, huku upinzani ukidai umeshinda uchaguzi huo.

Kwa usiku wa pili mfululizo, usalama umeimarishwa ndani na nje ya mji mkuu Harare. Maafisa wa polisi wameshika doria katika ngome za upinzani mjini humo wakiwa tayari kukabiliana na machafuko yoyote yanayoweza kutokea, huku kukiwa na wasiwasi kwamba rais Robert Mugabe anataka kuiba kura katika uchaguzi unaoelezwa kuwa muhimu zaidi tangu Zimbabwe ilipojipatia uhuru wake.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Marekani, Tom Casey, amesema Marekani inaitaka tume ya uchaguzi nchini Zimbabwe iyatangaze matokeo haraka. Kiongozi huyo anasema Marekani inachukua hatua kuhakikisha matokeo hayo yanadhihirisha kwa uwazi azma ya Wazimbabwe.

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa bunge yamekiweka chama cha rais Mugabe cha ZANU-PF katika nafasi ya pili nyuma ya chama cha Movement for Democratic Change, MDC, cha mpinzani wake mkuu, bwana Morgan Tsvangirai.

Huku matokeo ya uchaguzi wa rais yakisubiriwa, chama cha MDC kimedai kiongozi wake ameshinda kwa ailimia 60 kwa majibu wa matokeo yasiyo rasmi.

London kritisiert Moskaus Vorgehen gegen Kultureinrichtung
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza David MilibandPicha: picture-alliance/ dpa

Mwito wa nchi za Ulaya

Mawaziri wa mashauri ya kigeni wa nchi za Ulaya wanaokutana mjini Paris Ufaransa, wameitaka tume ya uchaguzi nchini Zimbabwe kutangaza haraka matokeo ya uchaguzi uliofanyika Jumamosi iliyopita.

Mawaziri hao kutoka nchi saba za Ulaya, zikiwemo Uingereza, Ufaransa na Uhispania, wamesema wanatarajia kufanya kazi pamoja na viongozi wa Zimbabwe watakaochaguliwa kwa njia ya demokrasia.

Matokeo kamili ya uchaguzi wa Zimbabwe bado hayajatangazwa.