1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu Afrika ya Kati aililia Ufaransa

Admin.WagnerD5 Desemba 2013

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Nicolas Tiangaye imetoa wito kwa Ufaransa kuharakisha kupeleka wanajeshi nchini mwake, baada ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha hatua hiyo.

https://p.dw.com/p/1ATa4
Gari la kijeshi likifanya doria mjini Bangui, baada ya kutokea mapigano usiku wa kumakia Alhamisi.
Gari la kijeshi likifanya doria mjini Bangui, baada ya kutokea mapigano usiku wa kumakia Alhamisi.Picha: Reuter/Emmanuel Braun

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kulipigia kura muda mfupi ujao, azimio la Ufaransa linaloidhinisha maelfu ya vikosi vya Afrika na Ufaransa kuingia nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambako mauaji ya kiholela yamezua hofu ya kutokea kwa mauaji ya halaiki. Waziri mkuu Nicolas Tiangaye, ambaye yuko mjini Paris kwa ajili ya Mkutano wa Ufaransa na mataifa ya Afrika, alisema kutokana na dharura iliyopo nchini mwake, angependa kuona uingiliaji kati unafanyika mara moja baada ya kupitisha azimio hilo.

Wapiganaji wa kundi la Kikristu la anti-balaka.
Wapiganaji wa kundi la Kikristu la anti-balaka.Picha: picture-alliance/AP

Wanajeshi zaidi wa Ufaransa kuwasili wiki hii
Tayari Ufaransa ina wanajeshi 600 katika koloni lake hilo la zamani, na leo 250 kati ya wanajeshi hao wamewekwa katikati mwa mji mkuu Bangui kufuatia ghasia zilizohusisha ufyatuaji risasi zilizotokea usiku wa kuamkia leo. Wanajeshi 600 zaidi wa Ufaransa wanatarajiwa kuwasili nchini humo mwishoni mwa wiki hii kukiongezea nguvu kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Afrika chenye jumla ya wanajeshi 2,500.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika machafuko baada ya waasi wa muungano wa Seleka, ambao wengi wao ni Wailsumu kumpindua rais aliekuwepo Francois Bozize mwezi Machi, ambapo Waislamu na Wakritu walianza kupigana wenyewe kwa wenyewe, na maelfu ya watu waliojawa na hofu kulaazimika kutafuta hifadhi katika makanisa na misikiti, wakihofia mashambulizi ya kimadhehebu.

Katika tukio la hivi karibuni la vurugu, milio mikubwa ya risasi iliibuka mjini Bangui, na ripoti zinasema watu wasipoungua 16 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa. Mapigano ya leo, yaliwahusisha kwa kiasi kikubwa, Waislamu wanaodhibiti taifa hilo lenye kiwango kikubwa cha umaskini, na Wakristu wanaomuunga mkono rais aliepinduliwa. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Laurent Fabius, ameonya kwamba nchi iko katika kingo za mauaji ya halaiki.

Fabius aliiambia televisheni ya BFM mapema leo, kwamba uingiliaji wa kijeshi utaanza mara moja baada ya kura ya Umoja wa Mataifa, na kwamba nchi yake itakuwa na jumla ya wanajeshi 1,200.

Waandamanaji wakiwa na bango limesalo 'Hapana kwa mauaji ya halaiki.'
Waandamanaji wakiwa na bango limesalo 'Hapana kwa mauaji ya halaiki.'Picha: Pacome Pabandji/AFP/Getty Images

Rais awaondoa hofu raia
Wakati huo huo, rais Michel Djotodia ametangaza leo kuongeza muda wa hali ya hatari katika mji mkuu Bangui kwa masaa manne, kuanzia saa 12 jioni, hadi saa 12 alfajiri, baada ya mapigano ya usiku wa kuamkia leo. Akiwasihi wakaazi wa mji wa Bangui kuendela kuwa watulivu katika hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja kupitia televisheni, Djotodia aliongeza kwamba jeshi la Ufaransa ni rafiki wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, na kuwataka raia wasiwe na hofu juu ya ujio wa jeshi hilo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, ape, dpae
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman