1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu mpya ateuliwa nchini Thailand

Eric Kalume Ponda15 Desemba 2008

Bunge la Thailand limemuidhinisha kliongozi wa chama cha upinzani cha Demokrat Abhisit Vejjajiva kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/GGht
Abhisit Vejjajiva, kiongozi wa chama cha Demokrat nchini Thailand achaguliwa kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo.Picha: AP


Vejjajiva mwenye umri wa miaka 44 anachukua mahala pa aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Somchai Wongsawat wa chama cha People Power PPP, kilichotimuliwa madarakani kufuatia uamuzi wa Mahakama mwanzoni mwa mwezi.


Uamuzi wa mahakama hiyo ulifuatia maandamano ya miezi mitatu ambayo kilele chake ilikuwa kuzingirwa na kufungwa kwa viwanja sita vya safari za ndege, ukiwemo uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bankok.


Hata hivyo hatua hiyo inapingwa vikali na wafuasi wa chama cha Peoples Power, hali inayozua hofu ya kuendelea kwa machafuko zaidi nchini Thailand.




Waziri mkuu huyo mpya alichaguliwa wakati wa kikao maalum cha bunge la nchi hiyo ambapo alishinda kwa wingi wa kura 235 dhidi ya mpinzani wake jemedari Pracha Promnok wa chama cha Puea Paendin kilichopata kura 198.


Abhisit Vejjajiva anakuwa waziri mkuu wa 27 akiwa na umri mdogo zaidi kuliongoza taifa hilo, ambalo linakumbwa na maandamano ya ghasia kuwahi kushuhudiwa katika muda wa miaka ya hivi karibuni.


Hatua hiyo imekirejesha madarakani chama hicho kikongwe zaidi kilichodumu kwa zaidi ya miaka 60 nchini Thailand na ambacho kimekuwa upande wa upinzani kwa muda wa miaka tisa sasa.


Wabunge wa chama hicho walisema wako tayari kuunda serikali katika muda wa wiki moja ijayo.

Hata hivyo serikali hiyo ni sharti iidhinishwe na Mfalme Bhumibol Adulyadej ambaye ni kiongozi wa taifa hilo kabla ya serikali hiyo kuanza kuhudumu.


Abhisit Vejjajiva hata hivyo anakabiliwa na changamoto nyingi ya kurejesha imani na hadhi ya taifa hilo katika ngazi za kimataifa, kufuatia msukosuko wa kisiasa na maandamano kutoka kwa kundi la upinzani la Peoples Alliance for Democracy PAD; yaliyopelekea kufungwa kwa uwanja wa ndege wa Bankok na kutatiza shughuli za uchumi wa taifa hilo.


Ingawa kundi hilo la PAD linasema kuwa litaunga mkono serikali ya Vejjjajiva, kundi jingine la upinzani limejitokeza kuipinga serikali hiyo mpya hali inayodidimiza matumaini ya kupatikana kwa sulughisho la mzozo wa kisiasa nchini Thailand.


Mamia ya waandamanaji waliovalia fulana nyekundu kutoka kundi linalodai kupinga utawala wa kiimla nchini humo, waliwashambulia na kuvunja vioo vya magari ya wabunge wa chama cha Demokrati walipokuwa wakiingia bungeni, wakiwashtumu kuwa baadhi yao walihusika na visa vya udanganyifu wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.


Makamu mkuu wa chama cha Demokrat Kraisak Choonhavan anasema Thailand huenda haitakuwa na serikali dhabiti iwapo katiba ya nchi hiyo aliyoitaja kuwa na mapungufu haitafanyiwa marekebisho.

Oton Kraisak Choonhavan......


Zaidi ya waandamanaji 200 wanaoinga mkono serikali ya waziri mkuu wa zamani Somchai Wongsawat walifunga barabara zinazoelekea majengo ya bunge. Waandamanaji hao yadaiwa ni wafuasi sugu wa aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Thaksini Shinawatra anayeishi uhamishoni ambaye alikuwa na ushawishi mkubwa katika serikali ya Somchai.


Chama cha PPP; kiliingia uongozini mwaka wa 2007 baada ya kushinda kwa jumal ya viti 232 dhidi ya viti 165 vilivyoshindwa na chama cha Democrat. Utawala wa Somchai ilipelekea maandamano na hatimaye mnamo tarehe 3 mwezi huu mahakama ilifutilia mbali serikali hiyo, hali iliyotoa nafasi kwa chama cha Demokrati kuvishawishi vyama vingine vidogo kuunda serikali.

Waziri huyo mpya amesema kuwa ajenda yake kuu ni kuimarisha uchumi wa taifa hilo uliozorota kufuatua ghasia hizo, ingawa alisita kuzungumzia zaidi hadi pale atakapoapishwa.


Sekta ya utalii ndiyo iliyoathiriika zaidi kufuatia ghasia hizo yilizopelekea mamaia ya watalii kukwama katika viwanja vya ndege nchini humo. Waandamanji hao walikuwa ameuzingira uwanja huo wa Bankok ili kumzuai waziri mkuu Somchai Wongsawat asirejee nyumbani kutoka mkutano wa kibiashara wa viongozi wa mataifa ya Asia na Pacific nchini Peru.