1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Armenia ajiuzulu

Caro Robi
23 Aprili 2018

Waziri mkuu wa Armenia Serzh Sargsyan amesema amejiuzulu ili kusaidia kudumisha amani katika taifa hilo lililokuwa la Kisovieti baada ya maandamano ya umma ya karibu kila siku tangu alipoingia madarakani Aprili, 17,2018.

https://p.dw.com/p/2wWWd
Armenien Ex-Präsident Sarkissjan trotz Protest zum Regierungschef gewählt
Picha: picture alliance/dpa/M. Metzel

Sargsyan, mshirika wa karibu wa Rais wa Urusi Vladimir Putin alihudumu kama rais wa Armenia kwa kipindi cha muongo mmoja hadi mapema mwezi huu na amekabiliwa na shutuma kali kutoka kwa umma dhidi ya mpango wa kutaka kung'angania madarakani wakati bunge lilipopiga kura kumchagua kuwa Waziri mkuu.

Mapema leo, shinikizo la kujiuzulu lilizidi dhidi ya mwanasiasa huyo wa miaka 63 baada ya wanajeshi wa Armenia waliokuwa hawana silaha kujiunga na maandamano ya kuipinga serikali katika mji mkuu Yerevan.

Taarifa ya  Sargsyan imesema alifanya makosa akiongeza katika hali ilivyo sasa, ana njia tofauti za kusuluhisha yanayojiri lakini hatotumia njia yoyote kati ya alizonazo kwani sio mfumo wake wa uongozi na hivyo ameamua kujiuzulu wadhifa wa Waziri mkuu wa Armenia.

Chini ya katiba iliyofanyiwa mageuzi, wadhifa wa Waziri mkuu sasa una mamlaka makubwa katika taifa hilo la Armenia ilhali wadhifa wa rais sasa kimsingi hauna mamlaka makubwa.

Nguvu ya umma yamuondoa Sargsyan madarakani

Wakazi wa mji mkuu wa Yerevan wamemiminika mitaani kusherehekea kujiuzulu kwa Sargaysan baada ya kuupinga utawala wake kwa siku kumi mfululizo. Maelfu ya waandamanaji wamekuwa wakiandamana mitaani tangu Aprili 13 na hapo jana maandamano hayo yalihudhuriwa na watu takriban 50,000.

Armenien Yerevan - Armenischer Premierminister Sargsyan trifft Oppositionsführer Pashinyan
Waziri mkuu wa Armenia Serzh Sargsyan na mpinzani Nikol PashinyanPicha: picture-alliance/dpa/TASS/A. Geodakyan

Kiongozi wa maandamano hayo Nikol Pashinian alikamatwa hapo jana baada ya kukutana na waziri mkuu huyo kwa mazungumzo. Hata hivyo leo mchana ameachiwa huru. Akiwahutubia wafuasi wake mjini Yereven, Pashiniyan amesema kila mmoja sasa ameelewa kuwa wameshinda.

Katika taarifa ambayo haikutarajiwa, Sargasyan amekiri kuwa hakupaswa kupinga matakwa ya upinzani akisema Niko Pashinian alikuwa sahihi na yeye alikosea.

Wakosoaji wa Sargasyan walimuona kama kiongozi anayejaribu kusalia madarakani baada ya ukomo wa muhula wake wa rais kukamilika. Armen Sarkisian, waziri mkuu wa zamani na balozi wa Armenia nchini Uingereza alichaguliwa kuwa rais.

Upinzani bado haujatoa tamko kuhusu kujiuzulu kwa Sargsyan na umeitisha maandamano leo jioni kati kati ya mji mkuu. Sargsyan, afisa wa zamani wa jeshi, alichaguliwa mara ya kwanza kuwa rais mwaka 2008 na kuchaguliwa tena mwaka 2013 kwa muhula wake wa pili na wa mwisho madarakani uliokamilika tarehe 9 mwezi huu wa Aprili.

Msemaji wa rais wa Urusi Vladimir Putin amesema Urusi inafuatilia kwa makini matukio yanayojiri Armenia. Dimtry Peskov amewaambia wanahabari kuwa Armenia ni muhimu sana kwa Urusi.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri:Yusuf Saumu