1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Iraq apania kuufufua ushirikiano wa kiuchumi na Ujerumani

23 Julai 2008

Ameyatolea mwito makampuni ya Ujerumani kuwekeza Iraq

https://p.dw.com/p/EiJE
Waziri mkuu wa Iraq Nouri al-MalikiPicha: picture-alliance/ dpa

Waziri mkuu wa Iraq Nuri al Maliki anakamilisha na ziara yake nchini Ujerumani hii leo.Jana alifanya mazungumzo na kansela Angela Merkel yaliyolenga zaidi katika masuala ya ushirikiano wa kiuchumi.Waziri mkuu wa Iraq amesema nchi yake iko salama na imerudi kwenye ulingo wa kibiashara.

Amesema anataka kuufufua uhusiano wa kihistoria wa kiuchumi na Ujerumani uliokuweko tangu miaka ya thamanini.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin waziri mkuu Nuri al Maliki amesema wamejitahidi na hatimae kufanikiwa kuikoa nchi yao kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kutokana na hali ya usalama kuimarika amesema wako tayari kuyakaribisha makampuni ya kigeni.

Kansela Angela Merkel kwa upande wake amebaini kwamba Ujerumani iko katika nafasi ya aina yake katika kuisaidia Iraq kujijenga upya nchi ambayo kwa sasa inahitaji kwa haraka wataalamu wa uhandisi na vifaa vya kiviwanda.

Amesema kuimarika kwa hali ya usalama nchini Iraq huenda kukafungua ukurasa mpya katika uhusiano kati ya pande hizo mbili.

Aidha Kansela Merkel amesema Iraq ni yenye utajiri wa mali ghafi nyingi na Ujerumani ina uwezo mkubwa katika masuala ya kitechnologia na kiviwanda na kwa maana hiyo amefarijika kuona kwamba baadhi ya makampuni ya Ujerumani yameshaonyesha nia ya kutaka kusaidia katika ujenzi mpya wa Iraq.

Waziri mkuu al Maliki ameitaka Ujerumani kuisaidia nchi yake katika nyanja za elimu,nishati endelevu na miundo mbinu.

Mwaka jana ujerumani ilisafirisha bidhaa za thamani ya euro millioni 319 katika nchi hiyo iliyosambaratishwa na vita lakini makampuni ya Ujerumani hivi sasa yako makini katika kuujenga uhusiano wa dhati wa kibiashara na taifa hilo.

Wakati huohuo nchini Iraq jana bunge la nchi hiyo liliidhinisha muswaada unaofungua njia ya kufanyika uchaguzi wa majimbo lakini wabunge wa kabila la wakurdi wameupinga muswada huoa kufuatia kutoelewana kuhusiana na suala la mzozo wa jimbo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Kirkuk.