1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte ajiuzulu

Amina Mjahid Gakuba, Daniel
20 Agosti 2019

Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte amewaambia wabunge wa nchi hiyo kwamba anajiuzulu kwa sababu kiongozi wa chama cha ligi Matteo Salvini kimeamua kuondoa uungaji mkono wake kwa serikali aliyoiongoza.

https://p.dw.com/p/3ODup
Italien Premierminister Giuseppe Conte im Oberhaus
Picha: picture-alliance/AP Photo/G. Borgia

Baada ya tangazo hilo bungeni Waziri Mkuu huyo Guiseppe Conte amesema  atakwenda kumfahamisha rasmi rais wa Italia Sergio Mattarella juu ya uamuzi wake.

Mattarella kama kiongozi wa nchi anaweza kumuomba Conte kuendelea kuwepo katika serikali hiyo changa ya miezi 14 na kujaribu kutafuta njia nyengine mbadala yakuwa na wingi wa kura bungeni au akubali uamuzi wa kujiuzulu kwake na kuona iwapo viongozi wengine wanaweza kupata namna ya kuunda serikali nyengine ya muungano.

Italien Regierungskrise | Innenminister Matteo Salvini in Rom
Waziri wa mambo ya ndani wa Italia Matteo Salvini Picha: Reuters/R. Casilli

Hilo likishindikana basi Mattarella anaweza kulivunja bunge na kufungua njia ya kuwa na uchaguzi mpya mapema kuanzia mwezi Oktoba.

Katika Hotuba yake bungeni hii leo Conte alimshutumu Matteo Salvini kwa kuweka maslahi yake binafsi na maslahi ya chama chake mbele kuliko yale ya taifa huku akionya kuwa hatua yake huenda ikauathiri uchumi wa taifa hilo.

Salvini kiongozi wa chama cha Ligi kinachopinga wahamiaji ameonekana kujiongezea umaarufu katika uchunguzi wa maoni wakati wa malumbano ya miezi kadhaa juu ya maamuzi muhimu ya kisera na mshirika wake katika serikali ya muungano ambao ni vuguvugu la nyota tano M5S.

Huenda uchaguzi mpya ukafanyika mwezo Oktoba

Salvini, ambaye pia ni naibu Waziri Mkuu anayetaka kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mapema anatarajiwa kushinda iwapo uchaguzi huo utaitishwa, hii ikiwa ni kulingana na uchunguzi wa maoni ya wapigakura nchini humo.

Italien Premierminister Giuseppe Conte im Oberhaus
Bunge la Italia Picha: picture-alliance/AP Photo/G. Borgia

Wiki mbili zilizopita kiongozi huyo wa chama cha Ligi nchini Italia alionesha nia yake ya kutaka kumalizika kwa serikali ya muungano na kundi lisilopenda utawala la vuguvugu la nyota tano, baadae aliubadilisha uamuzi wake huo lakini kundi hilo likasema hatua yake imekuja kuchelewa na hawawezi kurejesha mambo kama yalivyokuwa.

Kundi hilo sasa linatazamia kujaribu kuungana pamoja na chama cha upinzani cha Democratic Party.

Na iwapo hilo halitowezekana basi Italia italazimika kuandaa uchaguzi huo wamapema mwezi Octoba au Novemba au hata mapema mwaka 2020.

Vyanzo: rtre, afpe