1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Libya atimuliwa na bunge

Josephat Nyiro Charo12 Machi 2014

Waziri mkuu Ali Zeidan ametimuliwa na bunge jana (11.03.2014) baada ya meli ya mafuta kutoka bandari ya mashariki ya al Sidra kuzikwepa meli za jeshi la majini na kuingia eneo la kimataifa la bahari ya Mediterenia.

https://p.dw.com/p/1BNjH
Ali Seidan Ministerpräsident Libyen PK
Picha: Reuters

Muswada wa kutokuwa na imani na waziri mkuu Ali Zeidan ulipitishwa na wabunge 124 kati ya wabunge 194 wa bunge la taifa, ikiwa ni wabunge wanne zaidi kuliko idadi rasmi inayotakikana kikatiba. Taarifa ya bunge hilo imesema nafasi ya Zeidan imechukuliwa kwa muda na waziri wa ulinzi Abdullah al-Thani, ambaye aliapishwa jana mpaka waziri mkuu mpya atakapochaguliwa katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Zeidan alikuwa ameonya kwamba Libya itakabiliwa na machafuko iwapo ataondolewa bila kupatikana mtu wa kuchukua wadhifa wake. Lakini wabunge walighadhabishwa na kushindwa kwa serikali kutimiza vitisho vyake vya kuizuia meli hiyo kwa kutumia nguvu ikihitajika. "Serikali imedhoofishwa na tunahitaji kiongozi mpya," amesema mbunge huru, al-Sharif al-Wafi.

"Hali nchini haikubaliki. Hata wabunge waliokuwa wakimuunga mkono waziri mkuu hawana chaguo lengine tena," amesema Suad Gannur wakati alipozungumza na shirika la habari la AFP.

Zeidan aikimbia nchi licha ya marufuku

Mwendesha mashtaka mkuu wa serikali, Abdel-Qader Radwan, ameliambia shirika la habari la Reuters na televisheni ya Libya ya al-Ahrar kwamba amempiga marufuku Zeidan asisafiri nje ya nchi wakati atakapokuwa akichunguzwa. Hii ni kwa sababu anashukiwa kuhusika katika ubadhirifu wa fedha za umma, kwa mujibu wa waraka uliochapishwa kwenye ukurasa wa ofisi yake katika tovuti ya kijamii ya Facebook. Lakini vyombo vya habari vya Libya vimeripoti kwamba Zeidan alikuwa tayari ameondoka nchini humo.

Joseph Muscat
Waziri mkuu wa Malta, Joseph MuscatPicha: Thierry Charlier/AFP/Getty Images

Waziri mkuu wa Malta, Joseph Muscat ameiambia televisheni ya taifa kwamba Zeidan alikuwa Malta kwa muda wa masaa mawili jana jioni kabla kuelekea katika nchi nyingine ya Ulaya. Muscat amesema alizungumza naye kwa muda mfupi.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Jen Psaki, amesema Marekani itaendelea kuisadia serikali ya Libya iliyochaguliwa kwa njia ya demokrasia pamoja na watu wake. "Tuna shukrani kwa uongozi wa waziri mkuu ambaye alitawala wakati mgumu wa mpito wa Libya," akaongeza kusema Psaki.

Mapema jana meli yenye bendera ya Korea Kaskazini iliyokuwa imesheheni mafuta kutoka bandari inayodhibitiwa na waasi mashariki mwa nchi hiyo ilizikwepa meli za jeshi la majini zilizokuwa zimetumwa kuizuia isiondoke. Meli hiyo kwa jina Morning Glory iliyokuwa imetia nanga katika bandari ya al Sidra Jumamosi iliyopita na inayosemekana kubeba mapipa yapatayo 234,000, ni chombo cha kwanza kuwahi kuondoka bandari inayodhibitiwa na waasi tangu upinzani dhidi ya serikali ya Tripoli ulipoibuka mwezi Julai mwaka jana.

Msemaji wa jeshi la Libya amesema wanajeshi wa jeshi la majini la nchi hiyo waliifyetulia risasi meli ya Morning Glory na meli za Italia zinasaidia kuidhibiti meli hiyo ambayo kwa sasa imesimama.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE

Mhariri: Iddi Ssessanga