1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Pakistan azuru Afghanistan kwa mazungumzo ya amani

30 Novemba 2013

Waziri mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif anazuru Afghanistan hii leo(30.11.2013) kufanya mazungumzo na rais wa nchi hiyo Hamid Karzai kama sehemu ya juhudi za kufufua mchakato wa kutafuta amani nchini Afghanistan

https://p.dw.com/p/1AQu4
Picha: AFP/Getty Images

Ziara hiyo ya siku moja ni ya kwanza kufanywa na waziri huyo mkuu wa Pakistan nchini Afghanistan tangu achukue madaraka mwezi Mei na inakuja wakati ambapo rais Karzai anajikuta katika mzozo na Marekani kuhusu makubaliano muhimu ya kiusalama kuhusu kuendelea kusalia kwa wanajeshi wa Marekani baada ya kuondoka majeshi ya NATO mwaka ujao.

Pakistani inaonekana kuwa na usemi mkubwa katika kupatikana kwa amani katika nchi hiyo jirani kwani ilikuwa ikiunga mkono utawala wa wanamgambo wa Taliban kati ya mwaka 1996 hadi 2001 na inaaminika inawapa hifadhi baadhi ya viongozi wa kundi hilo la Taliban.

Jeshi la NATO kuondoka Afghanistan 2014

Wiki moja iliyopita,Sharif alikutana na ujumbe uliomtembelea kutoka baraza kuu la amani la Afghanistan ambalo linatafuta kuanzisha mazungumzo wazi na wanamgambo wa Taliban ambao wamekuwa wakikabiliana na wanajeshi wa jumuiya ya kujihami ya NATO wanaoongozwa na Marekani pamoja na wanajeshi wa Afghanistan tangu mwaka 2001.

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai,Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron na waziri mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif
Rais wa Afghanistan Hamid Karzai,Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron na waziri mkuu wa Pakistan Nawaz SharifPicha: RICHARD POHLE/AFP/Getty Images

Hivi karibuni, Pakistan ilimuachia huru kiongozi mwandamizi wa Taliban Mullah Baradar,anayeonekana na Afghanistan kama mtu muhimu atakayewashawishi wanamgambo hao kusogelea meza ya mazungumzo.

Lakini duru kutoka Taliban zinasema kundi hilo linalalamika kuwa kimsingi Baradar bado anazuiliwa nchini Pakistan na hakuna thibitisho kutoka baraza kuu la usalama kama liliweza kukutana naye lilipozuru Pakistan.

Karzai ambaye anatarajiwa kustaafu mwaka ujao kama rais wa Afghanistan amekuwa katika hali ya vuta nikuvute na Marekani kuhusu mkataba wa usalama utakaoruhusu jeshi la Marekani kusalia nchini humo baada ya mwaka ujao.

Vuta nikuvute kati ya Marekani na Karzai

Marekani inamshutumu Karzai kwa kutangaza masharti mapya katika dakika za mwisho kuhusu makubaliano hayo, licha ya baraza la viongozi wa kikabila wa Afghanistan la Loya Jirga kupiga kura ya kumuidhinisha kutia saini makubaliano hayo mara moja.

Wanamgambo wa Taliban
Wanamgambo wa TalibanPicha: Reuters

Machakato wa kutafuta amani Afghanistan umekwama tangu ofisi ya Taliban kufunguliwa nchini Qatar mwezi Juni hatua iliyomghadhabisha Karzai kwani ilipewa hadhi kama ubalozi wa serikali iliyo uhamishoni.

Kundi la Taliban limekataa kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na Karzai wala baraza hilo kuu la amani na kuwataja kuwa ni vikaragosi wa Marekani.Karzai na Sharif walikutana na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron mjini London mwezi Oktoba katika duru ya nne ya mikutano ya pande zote tatu inayopania kurejesha udhabiti katika eneo hilo la kusini mwa bara Asia.

Mwandishi:Caro Robi/afp

Mhariri: Sekione Kitojo