1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni miaka 20 ya kumbukubu ya mauaji ya Srebrenica

11 Julai 2015

Hasira yachemka Jumamosi (11.07.2015)katika kumbukumbu ya mauaji ya Srebrenica ya Waislamu wa Bosnia miaka 20 iliopita wakati watu walipomrushia mawe,chupa za maji na vitu vyengine Waziri Mkuu wa Serbia Aleksander Vucic.

https://p.dw.com/p/1FxHH
Kumbukumbu ya miaka 20 ya mauaji ya Srebrenica.
Kumbukumbu ya miaka 20 ya mauaji ya Srebrenica.Picha: Getty Images/AFP/D. Dilkoff

Msaidizi wa waziri mkuu huyo Suzana Vasilijevic ameliambia shirika la habari la AP kwamba miwani ya waziri mkuu huyo imevunjika wakati alipopigwa jiwe la uso.Vasilijevic amesema alikuwa nyuma ya Vucic wakati umma wa watu ulipovunja uzio na kuanza kuwageukia.

Maelfu ya watu walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya kumbukumbu hiyo ya miaka ya 20 ya mauaji mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa barani Ulaya tokea Maangamizi ya Kiyahudi ambapo wanaume na wavulana wa Kiislamu 8,000 waliuwawa katika mji wa mashariki wa Bosnia wa Srebrenica.Waheshimiwa wa kigeni waliohudhuria kumbukumbu hiyo wametowa wito kwa jumuia ya kimataifa kutoruhusu tena kuzuka kwa mauaji hayo ya kinyama na kuyaita kuwa ni mauaji ya kimbari.

Vucic ambaye aliwahi kuwa mwanasiasa wa sera kali za kizalendo amekwenda kuiwakilisha nchi yake katika kumbukumbu hiyo kwa kile inachoonekana kama ni ishara ya usuluhishi lakini imebidi aondoke kwenye kumbukumbu hiyo baada ya kushambuliwa.

Muadhara wa Vucic

Waziri wa mambo ya nje wa Serbia Ivica Dacic amesema shambulio hilo kwa Vucic lilikuwa ni shambulio kwa Serbia.Waziri huyo amesema katika taarifa kwa kuamuwa kuwainamia wahanga waziri mkuu huyo wa Serbia ameonyesha kitendo cha muungwana.Amesema hayo ni matokeo mengine mabaya ya kuliingiza siasa suala hilo jambo ambalo limesababisha kuzuka kwa mgawanyiko mpya na chuki badala ya upatanishi.

Wazir Mkuu Aleksandar Vucic akiweka shada la mawaua makaburini. (11.07.2015)
Wazir Mkuu Aleksandar Vucic akiweka shada la mawaua makaburini. (11.07.2015)Picha: Reuters/A. Bronic

Wakati Vucic alipoingia kuweka mauwa kwenye kaburi alizomewa na maelfu ya watu. Kuna waliomrushia kiatu, mawe, chupa za maji na vitu vyenginevyo na walinzi wake walijaribu kumhami kwa kutumia mikoba,miamvuli na kuonyesha juu sialaha zao.Ilibidi Vucic na walinzi wake wakimbie kwenye umma uliowakimbiza.

Baadhi wa waombolezaji walikuwa na mabango yenye kunukuu maneno ya waziri mkuu huyo aliyotowa wakati wa vita : "Kwa kila Mserbia mmoja atakayeuwawa tutawauwa Wabosnia 100."Serbia na Waserbia wa Bosnia wanakanusha muajia hayo kuwa ni ya kimbari na wanadai kuwa idadi ya mauaji imeongezwa chumvi.

Wageni waalikwa

Waheshimiwa kadhaa wa kigeni wamehudhuria kumbukumbu hiyo ya mauaji ya Waislamu wa Bosnia yaliofanywa na vikosi vya Serbia akiwemo Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu,Bintimfalme Anne wa Uingereza na Malkia Noor wa Jordan.Mauaji hayo baadae yalikuja kuelezewa kuwa ni mauaji ya kimbari na mahakama mbili za kimataifa.

Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton akizungumza wakati wa kumbukmbu ya miaka 20 ya mauaji ya Srebrenica. (11.07.2015)
Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton akizungumza wakati wa kumbukmbu ya miaka 20 ya mauaji ya Srebrenica. (11.07.2015)Picha: Reuters/D. Ruvic

"Nahuzunika kwamba imechukuwa muda mrefu kuungana kuzuwiya umwagaji damu huo " amesema hayo Rais wa zamani wa Marekani Bill Cinton ambaye alikuwa madarakani wakati mauaji hayo yakitokea na ni utawala wake ulioongoza mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo yaliokuwa yakishikiliwa na Waserbia.Hatua hiyo ndio iliokomesha vita vya Bosnia na kufikiwa kwa makubaliano ya amani yaliosimamiwa na Marekani.

Wakati wa vita hivyo vya mwaka 1992-1995 Umoja wa Mataifa ililitangzaa eneo la Srebrenica kuwa eneo salama kwa raia lakini hapo Julai 11 mwaka 1995 vikosi vya Serbia vililiteka eneo hilo la Waislamu.Wanaume 15,000 walijaribu kukimbilia misituni kuelekea kwenye maeneo yanayoshikiliwa na vikosi vya serikali wakati wengine waliungana na wanawake na watoto wa mji huo kutafuta hifadhi katika kambi ya vikosi vya Umoja wa Mataifa kutoka Uholanzi.

Uholanzi yabeba dhamana

Vikosi vya Uholanzi vilivyozidiwa nguvu vilikuwa vikiangalia tu wakati wanajeshi wa Serbia walipowachukuwa wanaume 2,000 kwa ajili ya kuwauwa na baadae kuwasaka na kuwauwa wengine 6,000 misituni.

Malkia Noor Al Hussein wa Jordan akisaini kitabu cha rambi rambi katika kumbukumbu ya miaka 20 ya mauaji ya Srebrenica. (11.07.2015)
Malkia Noor Al Hussein wa Jordan akisaini kitabu cha rambi rambi katika kumbukumbu ya miaka 20 ya mauaji ya Srebrenica. (11.07.2015)Picha: Reuters/S. Nenov

Umoja wa Mataifa umekiri kushindwa kwake kuwalinda watu wa mji huo na Bert Koenders waziri wa mambo ya nje wa Uholanzi amesema katika kumbukumbu hiyo kwamba serikali ya Uholanzi inabeba dhamana kwa yaliyotokea na kwamba Umoja wa Mataifa lazima uimarishe vikosi vyake kipindi cha usoni.

Vita vya Bosnia vya mwaka 1992 -1995 kati ya Waserbia Wakristo wa madhehebu ya Orthodox dhidi ya Waislamu wa Bosnia na Wakatoliki wa Croatia vimesababisha zaidi ya watu 100,000 kuuwawa na wengine mamilioni kupoteza makaazi yao Waserbia waliokuwa wakitaka kuendelea kubakia katika Yogoslavia inayoongozwa na Serbia walipambana dhidi ya kujitenga kwa Bosnia na Croatia kutoka shirikisho hilo lao la zamani.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri : Yusra Buwayhid