1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Ubelgiji afuta uwezekano wa kurudi madarakani.

Mohamed Dahman22 Desemba 2008

Waziri Mkuu wa Ubelgiji Yves Leterme amefuta uwezekano wa kurudi madarakani wakati tetesi za vyombo vya habari zikizidi kuongezeka kwamba Mfalme Albert amekuwa akijaribu kuifufuwa serikali iliosambaratika

https://p.dw.com/p/GLX7
Waziri Mkuu wa Ubelgiji Yves Leterme.Picha: AP

Hayo yanatokea wakati nchi hiyo ikikabiliwa na matatizo ya kiuchumi yanayohitaji utatuzi wa dharura.

Mfalme huyo wa Ubelgiji ambaye amekuwa na mashauriano na wanasiasa waandamizi bado kuamuwa iwapo akubali kujiuzulu kwa serikali hiyo.

Msemaji wa Leterme anasema waziri mkuu huyo anataka kulisafisha jina lake na yale ya wafanyakazi wake kwa tuhuma yoyote ile.

Leterme ameomba kujiuzulu kwa serikali yake hapo Ijumaa baada ya Mahkama Kuu kusema kwamba kuna dalili nzito za uingiliaji kati wa kisiasa katika kesi iliokuwa mahkamani juu ya mpango wa kunusuru taasisi ya kifedha ya Fortis wakati wa kilele cha mgogoro wa kifedha.

Taarifa ya Kasri la Mfalme imesema Mkuu wa chama cha Leterme cha Kiflemish cha Christian Demokratik Marianne Thyssen alikutana na mfalme hapo jana lakini haikutowa maelezo zaidi.Chama hicho ambacho ndio kikubwa kabisa bungeni kinatazamiwa kuamuwa nani atakuwa waziri mkuu.

Belgium ambako ndio yaliko makao makuu ya Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi NATO na Umoja wa Ulaya inatazamiwa kutumbukia kwenye mporomoko wa uchumi katika kipindi hiki cha robo mwaka na inahitaji kwa dharura serikali kuidhinisha mpango wa kuchochea uchumi wa euro bilioni 2 sawa na dola bilioni 2.8 na kufikia makubaliano juu ya mishahara pamoja na kutafuta ufumbuzi wa kuanguka kwa taasisi ya kifedha ya Fortis.

Wawekezaji wa Fortis ambao hisa zao zimeporomoka kwa takriban euro 1 kutoka kama euro 30 hao mwezi wa April mwaka 2007 wamefanikiwa kupinga kuanguka kwa taasisi hiyo na kuuzwa kwa mali zake kwa benki ya Ufaransa BNP Paribas.

Vyombo vya habari vya Ubelgiji ikiwa ni pamoja na tovuti ya De Morgen na magazeti ya De Standaard vimetowa hoja kwamba kwa vile hadi sasa mfalme amekuwa na mashauriano na wakuu wa vyama vitano tu tawala amewataka waendelee na mazungumzo.

Gazeti la lugha ya Kifaransa la Leo Soir limeongeza kusema kwamba kwa kuzingatia hali halisi kinachohitajika ni kuiweka upya serikali hiyo hiyo yenye wingi wa viti bungeni.

Masuala kuu mawili muhimu ni nani ataiongoza serikali na iwapo serikali hiyo itaweza kudumu kwa muhula kamili hadi mwaka 2011 au mwishoni mwa mwezi wa Juni mwaka 2009 wakati uchaguzi wa bunge unaweza kufanyika katika siku hiyo hiyo inayofanyika chaguzi za kanda na Umoja wa Ulaya.

Bado haiko wazi nani atamrithi Leterme.Waziri wa Fedha Didier Reynders amefuta uwezekano wa yeye kushika wadhifa huo mkuu.Rais wa baraza la chini la bunge Herman Van Rompuy mwenye umri wa miaka 61 imedokezwa kuwa anaweza kuchukuwa nafasi hiyo kwa kipindi cha muda mfupi.

Leterme aliomba kujiuzulu hapo mwezi wa Julai lakini mfalme wa Ubelgiji alimtaka aendelee kubakia baada ya kushindwa kufikia makubaliano kati ya vyama vinavyozungumza Kibelgiji ambavyo vilikuwa vikitaka madaraka zaidi kwa Waflender na wale wenye kuzungumza Kifaransa ambao walikuwa wakihofu kwamba hatua hiyo inaweza kuigawa Ubelgiji.

Waziri Mkuu huyo alihangaika kwa miezi tisa kuunda serikali na kushindwa mara mbili katika sakata ambalo lilizua tetesi za vyombo vya habari kwamba taifa hilo la miaka 178 linaweza kugawika pande mbili.