1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Ukraine awasilisha barua ya kujiuzulu

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
17 Januari 2020

Pendekezo la Waziri Mkuu huyo kutaka kuachia madaraka yake ni baada ya kuibuka mkanda wenye sauti yake inayosikika akimkosoa Rais Zelenskiy.

https://p.dw.com/p/3WN3h
Oleksiy Honcharuk Ukraine Premierminister
Picha: picture-alliance/dpa/Photoshot

Waziri Mkuu wa Ukraine Oleksiy Honcharuk ametangaza kujiuzulu na amefikisha rasmi kwa maandishi ombi lake hilo kwa Rais Volodymyr Zelenskiy siku ya Ijumaa (Januari 17). Waziri mkuu huyo amehudumu katika wadhifa huo katika muda wa chini ya miezi sita.

Kujiuzulu kwa waziri mkuu huyo wa Ukraine kumetokana na sauti iliyorekodiwa kwenye mkanda inayodaiwa kuibuka mapema wiki hii ambapo Honcharuk alisikika akihoji uwezo wa Zelenskiy katika kusimamia uchumi wa nchi hiyo jambo ambalo waziri mkuu ameliona kuwa linakiuka maadili ya wadhifa wake. Kwenye ujumbe aliouandika kwenye Facebook, Honcharuk alisema kuwa nafasi aliyopewa ilikuwa na lengo la kutimiza programu ya Rais Zelenskiy na kwamba kiongozi huyo kwake ni mfano wa uwazi na heshima. Barua ya kujiuzulu waziri mkuu huyo wa Ukraine inasubiri kuidhinishwa na ofisi ya rais ambayo ilijibu kwamba wangeizingatia.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS/P. Gonchar

Kabla ya kuwa waziri mkuu, Honcharuk alikuwa wakili katika ofisi ya waziri mkuu na ndiye alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Ukraine mwenye umri mdogo. Alikuwa na miaka 35 alipochukua jukumu hilo mnamo Agosti 2019.

Chanzo:/p.dw.com/p/3WL9C