1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Israel atilia ashaka juhudi za amani

Oumilkher Hamidou6 Septemba 2010

Avigdor Lieberman anasema haamini kama amani pamoja na wapalastina itapatikana "si kwa mwaka mmoja na wala si kwa kizazi kijacho"

https://p.dw.com/p/P5M4
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Israel Avigdor LiebermanPicha: AP

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Israel Avigdor Libermann amezusha ghadhabu ndani na nje ya Israel kutokana na matamshi yake yanayofifiisha matumaini ya kupatikana amani ya Mashariki ya kati.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Israel Avigdor Lieberman anasema amani haiwezi kupatikana kati ya waisrael na wapalastina katika kipindi kifupi kijacho.Katika mahojiano pamoja na vituo kadhaa vya habari nchini Israel,Avigdor Libermann anahisi"mazungumzo ya ana kwa ana yaliyoanza hivi karibuni pamoja na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas "hayataleta tija yoyote."Amemuonya waziri mkuu Benjamin Netanyahu dhidi ya kueneza matumaini kuhusu uwezekano wa kufanikiwa mazungumzo hayo.Akiwahutubia wafuasi wa chama chake cha siasa kali za kizalendo-Israel Beiteinu,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Israel Avigdor Lieberman amesema:

"Kutiwa saini makubaliano jumla ya amani,kumalizika mgogoro huu,kumalizika madai ya kila upande na kutambuliwa Israel kama taifa la umma wa wayahudi ni shabaha ambayo haitoweza kufikiwa sio mwaka huuu na wala si kwa kizazi kijacho."

Matamshi hayo yamezusha ghadhabu ndani na nje ya Israel.Waziri anaeshughulikia masuala ya jamii za wachache katika serikali ya muungano ya Israel, Avishai Braverman wa kutoka chama cha Labour amemtaka waziri mkuu Benjamin Netanyahu amuachishe kazi Lieberman kwa kutoa matamshi kama hayo.Ameiambia Radio ya Jeshi la Israel tunanukuu"si jambo linalokubalika kumuona mtu aliyepewa jukumu la kuwakilisha sera za Israel katika jumuia ya kimataifa akionyesha hali ya kutokua na imani na mazungumzo ya amani.

Mazungumzo ya ana kwa ana ya amani kati ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas yataendelea September 14 na 15 ijayo katika mji wa mwambao wa bahari ya Sham Charm el Sheikh.

Treffen im Weißen Haus Flash-Galerie
Mfalme Abdullah wa pili wa Jordan (kulia) akihudhuria mazungumzo ya amani pamoja na waziri mkuu wa Israel Benjamin NEtanyahu(kushoto),rais Hosni Mubarak wa Misri,rais Barack Obama na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud AbbasPicha: AP

Wakati huo huo mfalme Abdullah wa pili wa Jordan amekwenda Syria hii leo kumuarifu rais Bachar El Assad matokeo ya mazungumzo yake ya wiki iliyopita pamoja na rais Barack Obama wa Marekani,waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu,rais Hosni Mubarak wa Misri na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas.Jana mfalme Abdullah wa pili alionya" ulimwengu mzima utabeba jukumu pindi mazungumzo ya amani yakishindikana.

Mwandishi:Verenkotte,Clemens/ZR/Oummilkheir Hamidou

Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman