1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Ulinzi wa Marekani akutana na Waziri Mkuu wa Iraq

Kabogo Grace Patricia28 Julai 2009

Akiwa nchini Iraq, Waziri huyo Robert Gates, amesema amefurahishwa na hali ya usalama iliyopo kwa sasa.

https://p.dw.com/p/Iyxb
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates.Picha: AP

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates amepongeza maendeleo ya usalama nchini Iraq, katika ziara yake itakayoangalia masuala muhimu ikiwemo kuondoka kabisa kwa majeshi ya Marekani nchini Iraq na mauzo ya silaha. Waziri Gates pia atajaribu kuondoa mpasuko uliopo baina ya Wakurdi na Waarabu, ambao wengi wanahofia huenda wakadhoofisha juhudi za kurejea kwa hali ya usalama nchini humo.

Ikiwa ni ziara yake ya 10 kuitembelea Iraq, Bwana Gates amesema ameridhishwa na mabadiliko yaliyopo nchini humo. Akizungumza na maafisa wa usalama wa Iraq na Marekani katika kambi ya Tallil, Bwana Gates amesema hali ya usalama nchini Iraq iko tofauti ikilinganishwa na ilivyokuwa wakati alipozuru kwa mara ya kwanza nchi hiyo Desemba mwaka 2006.

Akiwa nchini humo, Waziri huyo wa ulinzi wa Marekani amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki, ambapo baadaye atakutana na Waziri wa Ulinzi, Abdel Qader Jassim na Jenerali Ray Odierno, kamanda wa juu wa Marekani nchini humo.

Bwana Gates amewasili mjini Baghdad akitokea katika eneo la kusini mwa nchi hiyo, baada ya ziara fupi ya Jordan na Israel. Akiwa nchini Israel Waziri Gates alisema silaha za nyuklia za Iran ni tishio kwa usalama wa eneo la Mashariki ya Kati.

Aidha, Bwana Gates atatembelea jimbo la Kurdistan lililopo kaskazini mwa Iraq, ambapo atafanya mazungumzo na Rais wa eneo hilo, Masoud Barzani, aliyesaini mikataba ya mafuta na kampuni za kigeni, hatua ambayo Waziri wa Mafuta wa Iraq, Hussain al-Shahristan anaichukulia kuwa ni kinyume cha sheria.

Ziara ya Waziri Gates nchini Iraq ni ziara ya pili ya afisa wa ngazi ya juu wa Marekani tangu vikosi vya Marekani kuondoka kutoka miji mikuu ya Iraq, Juni 30, mwaka huu. Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden alisherehekea siku ya uhuru wa Marekani, Julai 4 nchini Iraq. Ziara ya mwisho ya Bwana Gates nchini Iraq ilikuwa ni Septemba, mwaka 2008.

Ziara hii ya Bwana Gates inafanyika ikiwa ni wiki moja tangu Waziri Mkuu wa Iraq Nuri-al- Maliki alipokutana na Rais Barack Obama wa Marekani mjini Washington. Gates ana matumaini ya kuweka msisitizo wa mazungumzo baina ya Rais Obama na Al-Maliki, ambapo nchi hizo mbili zitakuwa na ushirikiano wa kawaida wakati majeshi ya Marekani yatakapoondoka Iraq.

Miongoni mwa mazungumzo hayo ni mabilioni ya dola ya Iraq yatakayotumika katika ununuzi wa silaha na nia ya Iraq kuwa na ndege za kivita za F-16 zinazotengenezwa na kampuni ya Lockheed Martin, kwa ajili ya kujihami na vitisho toka mataifa jirani, pindi majeshi ya Marekani yatakapoondoka nchini Iraq. Ufaransa, China na Urusi ni miongoni mwa nchi ambazo tayari zimeiuzia silaha Iraq.

Mwandishi: Garace Patricia Kabogo (RTRE)

Mhariri: M.Abdul-Rahman