Waziri wa Ulinzi wa Marekani Mattis ziarani china
27 Juni 2018Pamoja na maelewano hayo ya mazungumzo zaidi baina yao lakini kuna hali pia ya wasi wasi inayotokota pamoja na vita vya kibishara vinavyoelekea kukaribia.
Katika matamshi ya mwanzo kabla ya mkutano wa Mattis na rais wa China Xi Jinping pamoja na waziri wa ulinzi wa China Wei Fenghe, viongozi hao waliepuka kutaja chochote juu ya mada ambazo hapo kabla zilikuwa mbele katika uhusiano wao na kutafuta sehemu muhimu ya mazungumzo yao, masuala kama Taiwan, China kulifanya eneo la bahari ya kusini ya China kuwa la kijeshi pamoja na majadiliano yanayoendelea na Korea kaskazini kufikisha mwisho mpango wake wa kinyuklia.
Badala yake , walilenga katika umuhimu wa uhusiano wa kijeshi kati ya China na Marekani na vipi kuuendelea uhusiano huo. Waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis alisema.
"Nitarudia matamshi yako katika suala hili juu ya umuhimu unaowekwa katika ziara kati ya mataifa haya mawili, kuhusu ushirikiano wa kijeshi. Ndio sababu niko hapa, kujadili mfumo wa mkakati ambao kwa pamoja tunafanyakazi. Na nafikiri ni muhimu mno kwamba tuna majadiliano kama haya ya wazi, kwa kuangalia mbele katika njia ambayo tunaweza kushirikiana kila inapowezekana na kujadili tofauti zetu kama tunavyoweza baina ya mataifa yetu makubwa mawili."
Nia thabiti ya ulinzi wa mipaka na utaifa
Maelezo kuhusu mkutano wa Mattis asubuhi pamoja na waziri wa ulinzi Wei , yaliyotolewa na gazeti la kila siku la China , ilisema waziri wa ulinzi wa China aliweka msimamo wa China na wasi wasi wake kuhusu Taiwan, bahari ya kusini mwa China na Korea kaskazini, lakini halikutoa taarifa zaidi.
Wei alisisitiza kutokuwa na mzozo, bila mapambano, kuheshimiana na ushirika wa faida kwa pande zote pamoja na dhamira thabiti ya kijeshi katika ulinzi wa mipaka yake, usalama na maendeleo ya kimaslahi. Waziri wa ulinzi wa China Wei Fenghe alisema.
"Mheshimiwa waziri wa ulinzi , nafahamu kwamba ulikuwa mwanajeshi kwa miaka mingi na maneno yako yanabeba uzito wa kisiasa na katika duru za kijeshi."
Ziara ya Mattis pia inakuja huku kukiwa na vita vya kibiashara vikitokota baina ya mataifa hayo makubwa duniani kiuchumi. Rais Donald Trump tayari ameweka ushuru wa asilimia 25 kwa chuma cha pua kutoka China na asilimia 10 katika madini ya bati.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Yusuf Saumu