1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa zamani wa ulinzi Jung atiwa kishindo ajiuzulu

Oumilkher Hamidou27 Novemba 2009

Kadhia ya kuripuliwa malori ya mafuta huko Kunduz Afghanistan yapandisha mori za wabunge wa Ujerumani

https://p.dw.com/p/Khdi
Waziri wa zamani wa ulinzi,Franz Josef JungPicha: AP

Waziri wa zamani wa ulinzi,anaeongoza wizara ya kazi katika serikali mpya ya muungano wa nyeusi na manjano,Franz-Josef Jung amejitetea bungeni.Anasema hajaficha ripoti kuhusu malori mawili ya mafuta yaliyohujumiwa kwa mabomu na madege ya kivita huko Kunduz,kaskazini mwa Afghanistan.

Waziri wa kazi wa serikali kuu ya ujerumani,Franz-Josef Jung hatojiuzulu.Katika hotuba yake iliyokua ikisubiriwa kwa hamu bungeni, waziri huyo wa zamani wa ulinzi amezisuta dhana zote anazotupiwa kwamba amelihadaa bunge na hadhara ya Ujerumani.

Vituo husika nchini Afghanistan vimemhakikishia katika hujuma hiyo dhidi ya malori mawili ya mafuta yaliyoibiwa,hakuna raia wa kawaida aliyeuliwa.Mapema mwezi October,mkuu wa vikosi vya wanajeshi,Jenerali Wolfgang Schneiderhan alimuarifu kuhusu ripoti ya polisi ya kijeshi kuhusu kadhia hiyo ambayo waziri Jung anasema ameituma kwa uongozi wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO.

"Kwangu mie ilikua muhimu kwamba watu wanaarifiwa juu ya uchunguzi wote uliofanywa na NATO.Ndio maana nimetoa ruhusa.Lakini kilichoandikwa hasa ndani ya ripoti hiyo sikuarifiwa."

Siku moja tuu baada ya shambulio hilo lililogharimu maisha ya watu 142,anasema alizungumzia kwa masikitiko juu ya uwezekano wa raia kuangukia mhanga wa shambulio hilo.Kwa namna hiyo anasema waziri Jung,anaamini uamuzi wake ulikua sawa na hakua na dhamiri ya kulificha bunge wala jamii ya Ujerumani.

Flash-Galerie Wochenrückblick KW 48 Franz Josef Jung
Waziri wa sasa wa kazi,anatiwa kishindo ajiuzuluPicha: AP

Upande wa upinzani umekasirishwa na hoja za waziri Jung.Mtaalam wa masuala ya ulinzi kutoka chama cha SPD, Rainer Arnold amemtaka waziri Jung abebe jukumu la yaliyotokea.

Mkuu wa kundi la walinzi wa mazingira Die Grüne Jürgen Trittin amekosoa ile hali kwamba waziri Jung amechukua ripoti ya polisi ya kijeshi na kuipelekea jumuia ya kujihami ya magharibi NATO,bila ya kuzipelekea kamati maalum za sio ile inayoshughulikia masuala ya ulinzi na wala si ya mambo ya nchi za nje.

"Sio tuu hujasema ukweli,lakini pia umetudaganya.....na hali hiyo ni kinyume na demokrasia."

Walinzi wa mazingira na makundi mengine ya upande wa upinzani yanataka kamati ya ulinzi ya bunge iunde tume ya uchunguzi ili kuchunguza kadhia hiyo.Mkuu wa chama cha mrengo wa shoto-Die Linke anahisi,mwishoe waziri Jung hatokua na njia nyengine isipokua kujiuzulu.

Kansela Angela Merkel hadi wakati huu amejaribu kumuepuka waziri Jung.Katika mkutano na waandishi habari pamoja na katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO,Anders Fogh Rasmussen,kansela Angela Merkel amesema daima amekua akithamini uwazi.Amesema anamuunga mkono waziri wa ulinzi Zu Guttenberg katika juhudi zake za kumulika na kufafanua kadhia hiyo.

Mwandishi: Marx,Bettina/ZR/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Abdul-Rahman