1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Westerwelle akamilisha ziara yake Mashariki ya Kati

Josephat Nyiro Charo24 Mei 2010

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amerejea Ujerumani leo baada ya kukamilisha ziara yake ya Mashariki ya Kati

https://p.dw.com/p/NVaC
waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Guido Westerwelle, kulia, na rais wa Syria Bashar AssadPicha: AP

Siku ya mwisho ya ziara yake hapo jana, bwana Westerwelle alikutana na rais wa Syria, Bashar al Assad, mjini Damascus na kuitaka Syria iunge mkono mazungumzo kati ya Israel na Wapalestina ili ipatiwe msaada wa kiuchumi.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema mchakato wa kutafuta amani ya Mashariki ya kati sio tu swala linalozusha wasiwasi katika eneo hilo pekee, bali ni kitendawili kinachowaumiza vichwa viongozi wa kimataifa. Westerwelle amesisitiza haja ya kufanyika mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Israel na Wapalestina huku akiahidi kufanya kila jitihada kuzihimiza pande zote husika ili kuhakikisha mazungumzo hayo yanafanyika.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi habari mjini Damascus akiwa ameandamana na waziri wa mambo ya kigeni wa Syria, Walid al Moallem, waziri Westerwelle amesema Syria ina jukumu muhimu katika kufikia suluhisho la maana la mzozo wa Mashariki ya Kati. Westerwelle ameongeza kuwa yeyote anayetaka kusaidia mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati lazima atafute ushirikiano na Syria. Hata hivyo amesema Ujerumani inataraji kwamba Syria itakuwa tayari kuziunga mkono pande zinazoshiriki katika juhudi za kuutanzua mzozo wa Mashiriki ya Kati.

Syria, kituo cha mwisho cha ziara ya Westerwelle Mashariki ya Kati, ndicho pengine kilichokuwa muhimu zaidi. Nchi za magharibi zimeelezea wasiwasi wao kuhusu jukumu la Syria katika eneo hilo, huku zikipinga hatua ya nchi hiyo kulisaidia kundi la Hamas la Palestina na Hezbollah nchini Lebanon, ambalo Israel inasema linapokea makombora kutoka Syria.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Syria, Walid al Moallem amesema silaha za aina hiyo haziwafai wapiganaji wa Hezbollah kwa sababu ya mbinu wanazotumia. Al Moallem aidha amesema Syria inazikaribisha juhudi za Umoja wa Ulaya kuunga mkono mazungumzo ya ana kwa ana baina Israel na Syria yanayosimamiwa na Uturuki.

Guido Westerwelle zu Besuch in Syrien im Gespräch mit Walid Al-Moallem
Waziri wa kigeni wa Ujerumani Guido Westerwelle, kulia, na waziri wa kigeni wa Syria Walid Al-MoallemPicha: AP

Wakati wa ziara yake ya Mashariki ya Kati iliyompeleka pia nchini Misri, Jordan na Lebanon, waziri Westerwelle alikutana na viongozi wa kiarabu na kurudia mwito wake kuitaka Israel na Wapalestina waondokane na mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana yanayosimamiwa na Marekani, na badala yake waanze mashauriano ya moja kwa moja.

"Tumekubaliana kwamba sasa ni wakati wa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana. Hiyo ina maana tunalazimika sasa kuweka mazingira yatakayowezesha mazungumzo hayo kufanyika na muda uliosalia kufanyika mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana lazima utumike vyema kabisa. Pande husika katika mzozo huu zinatakiwa kubeba dhamana na kuwepo uongozi unaofaa wa mchakato mzima, bila shaka kupitia mataifa jirani."

Wakati alipokuwa mjini Amman Jordan mapema jana, Westerwelle alifanya mkutano na waandishi habari akiwa ameandama na mwenyeji wake waziri wa mambo ya kigeni wa Jordan, Nasser Judeh. Waziri Judeh alieleza matumaini yake kuhusu mazungumzo yanayoendelea hivi sasa kati ya Israel na Wapalestina akisema kwa muda mrefu watu wamekuwa wakisubiri amani Mashariki ya Kati

"Watu wengi katika eneo hili ni vijana na wamenyimwa nafasi walizonazo vijana wengine ulimwenguni kwa miaka mingi. Wakati umewadia kwa sisi sote kushirikiana kuhakikisha kuna amani katika eneo hili."

Westerwelle amesema Jordan, ambayo ilisaini mkataba wa amani na Israel takriban miaka 15 iliyopita, ina jukumu kubwa katika juhudi za kutafuta amani ya Mashariki ya Kati na kuishukuru kwa jitihada zake.

Ziara ya Westerwelle ililenga kuchunguza vipi Ujerumani inavyoweza kuchagia juhudi za kuupiga jeki mpango wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati.

Mwandishi:Kühntopp,Carsten/Amman (WDR)/Charo, Josephat

Imepitiwa na: Hamidou Oummilkheir