1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Westerwelle ataka uhusiano wa Ujerumani na Ufaransa uimarishwe

3 Novemba 2009

Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle yuko katika ziara ya kujitambulisha, katika mataifa mbalimbali, ambapo jana alikuwa Ufaransa na Uholanzi.

https://p.dw.com/p/KM47
Waziri wa Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle,Picha: AP

Akiwa mjini Paris alikuwa na mazungumzo na Rais Nicolaus Sarkozy wa Ufaransa ambapo alielezea umuhimu wa kuimarishwa kwa  uhusiano maalum kati ya mataifa hayo mawili kwa manufaa ya Ulaya.

Akizungumza mara baada ya kukutana na Rais Sarkozy pamoja na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Fillon, Bwana Westerwelle alisema kuwa  uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa ni wa kiasili na kwamba anaipenda Ufaransa.

´´Siku zote nimekuwa nikiihusudu na kuipenda Ufaransa.Kwa kizazi changu, makuzi yetu yamekuwa pamoja kutokana na kazi za vijana kupitia mpango wa kubadilishana vijana kati ya Ufaransa na Ujerumani.Hili ni lazima lisiwe tena somo bandia.Uhusiano huu kati ya Ujerumani na Ufaransa uko ndani ya damu yetu, na hili pia ni zuri kwetu´´  .

Waziri huyo wa Nje wa Ujerumani alisisitiza kuwa uhisiano kati ya mataifa hayo mawili ni nguvu kubwa ya Umoja wa Ulaya, hivyo akasema ni muhimu uimarishwe kwa manufaa ya eneo hilo.

Guido Westerwelle in Frankreich
Waziri wa Nje wa Ufaransa Bernard Kouchner,kulia na mgeni wake Guido WesterwellePicha: AP

KOUCHNER

Mapema alikuwa na mazungumzo na Waziri mwenziye wa nje wa Ufaransa Bernard Kouchner, ambapo alimwambia waziri huyo wa Ufaransa kuwa  yuko tayari kushirikiana naye akimtaja kuwa ni mtu makini na mwenye uwezo ambaye amefanya mengi katika siasa.Waziri Kouchner alikuwa akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa kutimiza miaka 70.

´´Tunataka pia tuwe tunawasiliana kwa njia ya simu kila wiki, kujadiliana masuala mengine  tuliyoyaweka pembeni, na hii si tu masuala yanayohusu siasa za Ulaya, bali pia nje ya hapo´´

AFGHANISTAN

Akizungumzia suala la Afghanistan Bwana Westerwelle ambaye pia ni Naibu Kansela,  alielezea matumaini yake kwa serikali mpya ya Rais Karzai kufanyakazi kwa manufaa ya watu wote wa Afghanistan.

´´Changamoto  anayokabiliana nayo rais mpya ni kubwa.Kuijenga upya Afghanistan.kuimarisha usalama na kupambana na rushwa.Tunategemea atayatekeleza haya.Tunategemea pia atafanya juhudi za kuyaunganisha makundi mbalimbali ya jamii ya wananchi wa Afghanistan na atakuwa rais wa wananchi wote wa Afghanistan´´

Westerwelle in Polen
Guido Westerwelle,kulia na Rais wa Poland Lech KaczynskiPicha: AP

Imekuwa ni utaratibu kwa viongozi wapya wa Ujerumani kuanza kuitembelea Ufaransa kwanza, kabla ya nchi nyingine yoyote.Lakini Guido Westerwelle alianza kuitembelea  Poland kabla ya kuelekea Ufaransa.

Leo waziri huyo mpya wa nje wa Ujerumani atazitembelea, Ubelgiji na Luxembourg, kabla ya hapo kesho kuelekea Washington Marekani ambako atakuwa na mazungumzo na waziri mwenziye wa nje Bibi Hillary Clinton.

Mwandishi:Angela Ulrich

Mtafsiri:Aboubakary Liongo

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman